Arsenal wakomoa Watford na kuingia tano-bora EPL

Arsenal wakomoa Watford na kuingia tano-bora EPL

Na MASHIRIKA

ARSENAL waliendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mechi 10 mfululizo kwenye mapambano yote ya msimu huu baada ya kuwatandika Watford 1-0 katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Emirates, Jumapili.

Wanabunduki wa Arsenal waliofungiwa na Emile Smith Rowe katika dakika ya 56, walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 2-0 katika mchuano wa awali wa EPL dhidi ya Leicester.

Watford ya kocha Claudio Ranieri ilikuwa ikipania kujinyanyua baada ya kuzamishwa 1-0 na Southampton wiki moja iliyopita.

Ushindi huo ulirejesha Arsenal katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 20, sita pekee nyuma ya viongozi Chelsea na tatu chini ya mabingwa watetezi Manchester City.

Mabingwa mara 20 wa EPL, Manchester United wanasoma mgongo wa Arsenal kwa alama 17 ambazo pia zinajivuniwa na nambari saba Brighton.

Miezi miwili iliyopita, Arteta alijipata katika presha kubwa ya kupigwa kalamu na Arsenal waliopoteza mechi tatu za kwanza ligini na wakajikuta wakikokota nanga mkiani mwa jedwali.

Walitandikwa na Brentford (2-0), Chelsea (2-0) na Man-City (5-0) kabla ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Norwich City na Burnley kuashiria mwanzo wa ufufuo wa makali yao.

Tangu wakati huo, Arsenal waliopepeta Spurs 3-1 mnamo Septemba 26, wamepoteza alama nne pekee ligini baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya Brighton na kukabwa koo 2-2 na Crystal Palace.

Mabingwa hao mara 13 wa EPL wameshinda mechi sita na kupoteza tatu kati ya 11 zilizopita.

Walikomoa Aston Villa 3-1 kabla ya kuvuruga mipango ya Leicester na Watford kwa usanjari huo. Sasa wanajiandaa kumenyana na Liverpool, Newcastle United, Man-United, Everton, Southampton na West Ham United kwa usanjari huo.

Kuhusu mechi ya Jumapili, Arsenal walipoteza nafasi maridhawa ya kujiweka uongozini na kupunguza presha kutoka kwa Watford katika dakika ya 36 baada ya penalti ya nahodha na mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang kupanguliwa na kipa Ben Foster.

Mkwaju huo ulitokana na tukio la fowadi Alexandre Lacazette kuchezewa visivyo na beki Danny Rose ndani ya kijisanduku.

Watford walikamilisha mchuano huo na wachezaji 10 uwanjani baada ya kiungo raia wa Slovakia, Juraj Kucka kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Mlinda-lango wa Arsenal, Aaron Ramsdale naye alifanya kazi ya ziada na kudhibiti vilivyo makombora mazito aliyoelekezewa na wavamizi wa Watford ambao kwa sasa wamejizolea alama 10 kutokana na mechi 11 zilizopita ligini.

Alama za Watford wanaokamata nafasi ya 17, zinawiana na za Aston Villa waliomfuta kazi kocha Dean Smith hapo jana baada ya kujivunia huduma zake kwa miaka mitatu.

Smith, 50, anaondoka Villa baada ya Southampton kuwatandika 1-0 katika EPL mnamo Ijumaa ugani St Mary’s. Hiyo ilikuwa mechi ya tano mfululizo kwa Villa kupoteza kwenye EPL msimu huu.

Arsenal wananolewa na kocha Mikel Arteta, wangalifunga mabao zaidi katika kipindi cha pili kupitia Aubameyang, Kieran Tierney, Lacazette na Bukayo Saka ambaye nafasi yake ilitwaliwa na Gabriel Martinelli dakika nane kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Mara ya mwisho kwa Watford kuondoka ugani Emirates na alama tatu kapuni ni Januari 2017 baada ya kucharaza Arsenal 2-1 katika mchuano wa EPL.

Mechi ya Jumapili ilikuwa yao ya tano kwa Watford kupoteza kutokana na sita zilizopita dhidi ya Arsenal ambao hawajawahi kukamilisha mechi dhidi ya wapinzani wao hao bila kufunga goli.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Aston Villa wamtimua kocha Dean Smith kwa sababu ya matokeo...

Raila kutangaza ikiwa atawania urais Desemba 9

T L