Arsenal wakung’uta Leicester City katika mechi ya EPL ugani King Power

Arsenal wakung’uta Leicester City katika mechi ya EPL ugani King Power

Na MASHIRIKA

ARSENAL waliendeleza ufufuo wa makali yao msimu huu kwa kuzamisha Leicester City 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hapo jana uwanjani King Power.

Masogora wa kocha Mikel Arteta walichuma nafuu tele kutokana na utepetevu wa wenyeji wao katika kipindi cha kwanza na wakafunga mabao mawili ya haraka kupitia Gabriel Magalhaes na Emile Smith Rowe chini ya dakika 20 za mwanzo wa kipindi cha kwanza.

Arsenal kwa sasa hawajashindwa katika mechi saba zilizopita za EPL na wanajivunia alama 17, sawa na West Ham United watakaochuana na Aston Villa leo ugenini. Ni pengo la pointi tatu ndilo linalotamalaki kwa sasa kati ya Arsenal na Leicester ya mkufunzi Brendan Rodgers.

Licha ya kujivunia idadi kubwa ya mashabiki wa nyumbani, Leicester walishindwa kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakikung’uta Manchester United (4-2) na Brentford (2-1) katika mechi mbili za awali ligini.

Hata hivyo, walivamia Arsenal kwa muda mrefu katika kipindi cha pili na kumweka kipa Aaron Ramsdale katika ulazima wa kujituma maradufu na kudhibiti makombora mazito aliyoelekezewa na James Maddison, Jamie Vardy, Ademola Lookman, Patson Daka, Kelechi Iheanacho na Youri Tielemans.

Baada ya kumenyana na Watford katika mchuano wao ujao ligini, Arsenal watapepetana na Liverpool, Newcastle United, Manchester United na Everton kwa usanjari huo. Leicester watakwaruzana na Spartak Moscow katika Europa League Alhamisi ijayo kabla ya kuonana na Leeds United na Chelsea ligini.

You can share this post!

Wakazi walia kucheleweshewa soko

Familia ya msomi wa kiislamu aliyetekwa nyara sasa yamtaka...

T L