Arsenal wapepeta Southampton na kutinga ndani ya orodha ya 8-bora EPL

Arsenal wapepeta Southampton na kutinga ndani ya orodha ya 8-bora EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta amesema kwamba ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na vijana wake wa Arsenal dhidi ya Southampton mnamo Jumanne usiku ugani St Mary’s ni zawadi spesheli kwa nahodha Pierre-Emerick Aubameyang aliyekosa mechi hiyo kwa sababu za kibinafsi.

Licha ya kutokuwepo kwa Aubameyang ambaye ni raia wa Gabon, Arsenal walishinda Southampton kirahisi baada ya kuweka kando maruerue ya kuondolewa kwao na kikosi hicho kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA wikendi iliyopita kwa kichapo cha 1-0 uwanjani St Mary’s.

Baada ya fowadi Alexandre Lacazette kupoteza fursa nzuri ya kuwaweka Arsenal kifua mbele katika dakika ya kwanza, Stuart Armstrong aliwapa Southampton uongozi kwa kukamilisha krosi ya nahodha James Ward-Prowse.

Hata hivyo, uongozi huo wa The Saints ulidumu kwa dakika tano pekee kabla ya Nicolas Pepe kusawazisha mambo kwa upande wa Arsenal.

Vikosi vyote viwili vilicheza kwa kushambulia sana huku beki Cedric Soares ambaye ni mchezaji wa zamani wa Southampton akichangia krosi nyingi ambazo zilichangia ari ya Arsenal waliosalia kumtegemea pakubwa kipa Bernd Leno kupangua makombora kadhaa aliyoelekezewa na mshambuliaji Danny Ings na kiungo Che Adams.

Kiungo chipukizi raia wa Uingereza, Bukayo Saka aliwaweka Southampton uongozini baada ya kumzidi ujanja kipa Alex McCarthy katika dakika ya 39.

Saka, 19, alichangia bao la tatu la Arsenal lililofungwa na Lacazette katika dakika ya 72.

“Aubameyang anapitia hali ngumu na sote tuko nyuma yake. Ushindi huu ni kwa ajili yake,” akasema Arteta kumhusu fowadi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ambaye pia hakuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Arsenal dhidi ya Southampton kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA mnamo Januari 23, 2021.

Walipolazimishiwa sare ya 1-1 kutoka kwa Southampton katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa EPL uwanjani Emirates mnamo Disemba 16, 2020, Arsenal walikuwa katika nafasi ya 15 na ni pengo la alama 10 ndilo lilikuwa likitenganisha vikosi hivyo kwenye msimamo wa jedwali.

Chini ya kocha Ralph Hasenhuttl, Southampton kwa sasa wanashikilia nafasi ya 11 kwa alama 29 sawa na Chelsea na Aston Villa.

Kwa upande wao, Arsenal walichupa hadi nafasi ya nane kwa alama 30, tano nyuma ya West Ham United ambao chini ya kocha David Moyes, wanafunga sasa mduara wa nne-bora.

Ushindi wa Arsenal ulikuwa wao wa tano kati ya mechi sita zilizopita ligini. Ufanisi huo dhidi ya Southampton unatarajiwa sasa kuwapa motisha zaidi ya kuvaana na Manchester United watakaokuwa wageni wao kwa minajili ya gozi la EPL mnamo Januari 30 ugani Emirates.

Ni Manchester City ambao wamejizolea idadi kubwa ya alama (18) na kufungwa idadi ndogo ya mabao (moja) kuliko Arsenal tangu Disemba 26, 2020.

Arsenal kwa sasa wako pua na mdomo kukamilisha uhamisho wa chipukizi Martin Odegaard kwa mkopo kutoka Real Madrid. Southampton watakuwa wenyeji wa Aston Villa katika mchuano wao ujao wa EPL mnamo Januari 30.

You can share this post!

Raila atarajiwa Githurai kupigia debe BBI

Kocha Thomas Tuchel aanza kazi kambini mwa Chelsea baada ya...