Arsenal waponda Norwich City na kumtia kocha Dean Smith kwenye presha ya kutimuliwa

Arsenal waponda Norwich City na kumtia kocha Dean Smith kwenye presha ya kutimuliwa

Na MASHIRIKA

ARSENAL walishinda mechi yao ya nne mfululizo katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuzamisha chombo cha Norwich City kwa mabao 5-0 mnamo Jumapili uwanjani Carrow Road.

Ushindi huo wa masogora wa kocha Mikel Arteta ulirefusha mkia wa Norwich kwenye msimamo wa jedwali la EPL na kuwaweka katika hatari zaidi ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za muhula huu.

Bukayo Saka alifungulia Arsenal karamu ya mabao katika dakika ya sita kabla ya Martin Odegaard aliyechangia goli la kwanza kuchangia jingine lililofumwa wavuni na Kieran Tierney katika dakika ya 44.

Saka aliongeza goli lake la pili na la tatu kwa upande wa Arsenal katika dakika ya 67 kabla ya Alexandre Lacazette kufunga penalti ya dakika ya 84 kisha Emile Smith Rowe aliyetokea benchi kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao.

Arsenal walidumisha nafasi yao ya nne kwenye msimamo wa jedwali la EPL na sasa wanajivunia pengo la alama sita kati yao na Tottenham Hotspur wanaokamata nafasi ya tano kwa alama 29, moja zaidi kuliko West Ham United waliocharazwa na Southampton 3-2.

Kichapo cha Norwich kilikuwa chao cha 12 kutokana na mechi 18 za hadi kufikia sasa msimu huu na sasa wanakokota nanga kwa alama 10 sawa na Newcastle United.

Mechi hiyo ilimpa Arteta fursa ya kuadhimisha miaka miwili tangu apokezwe mikoba ya Arsenal. Arsenal walikuwa wakishikilia nafasi za 11 na 14 kufikia Disemba 26, 2019 na 2020 mtawalia. Sasa wameimarika pakubwa huku wakiweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara wa nne-bora kwa mara ya kwanza tangu 2016.

Norwich kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Crystal Palace katika mchuano mwingine wa EPL mnamo Disemba 28, 2021 japo maandalizi yao yamevurugwa na Covid-19 ambayo iliyomnyima kipa tegemeo Tim Krul fursa ya kuwajibika dhidi ya Arsenal.

Chini ya kocha Dean Smith, Norwich kwa sasa hawajafunga bao lolote kutokana na mechi nne zilizopita huku wakijivunia mabao manane pekee kapuni mwao baada ya mechi 18 za hadi kufikia sasa ligini msimu huu.

Teemu Pukki ambaye ni mfungaji bora wa Norwich aligusa mpira mara 23 pekee dhidi ya Arsenal.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Harry Kane aongoza Spurs kupepeta Crystal Palace katika...

Martial asema huu ndio wakati mwafaka zaidi kwake kuondoka...

T L