Michezo

Arsenal waponea chupuchupu kulazwa na Leeds United baada ya Pepe kuonyeshwa kadi nyekundu

November 23rd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

FOWADI wa Nicolas Pepe alionyeshwa kadi nyekundu katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyoshuhudia waajiri wake Arsenal wakiponea chupuchupu kuzamishwa na Leeds United mnamo Novemba 22, 2020 uwanjani Elland Road.

Vijana wa kocha Marcelo Bielsa waliokuwa wenyeji wa mechi hiyo walipoteza nafasi nyingi za wazi kabla na baada ya Pepe kufurushwa ugani kwa kosa la kumpiga kwa kichwa kiungo Ezgjan Alioski.

Wachezaji Moreno Rodrigo, Patrick Bamford na Raphinha Belloli walishuhudia makombora yao katika kipindi cha pili yakigonga mwamba wa goli la Arsenal waliosalia kumtegemea pakubwa kipa Bernd Leno.

Arsenal walitepetea pakubwa katika mechi hiyo huku jaribio la pekee walilolipata langoni pa wenyeji wao likitokana na fataki mbili zilizopigwa na Pierre-Emerick Aubameyang katika dakika ya 60 na 77.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal kwa sasa wamfunga bao moja pekee la EPL, penalti iliyopachikwa wavuni na Aubameyang dhidi ya Manchester United, katika jumla ya mechi tano zilizopita tangu Oktoba 4, 2020.

Arsenal na Leeds waliingia ugani kwa minajili ya mchuano huo kila mmoja akitarajia kujinyanyua baada ya kupoteza mechi tatu kati ya nne za awali ligini.

Sare dhidi ya Leeds United iliwasaza Arsenal katika nafasi ya 11 kwa alama 13 sawa na Crystal Palace, Manchester United na Wolves. Ni pengo la alama mbili pekee ndilo linalotamalaki kati ya Arsenal na Leeds ambao wanashikilia nafasi ya 14 kwa pointi sawa na Newcastle United.

Leeds ndicho kikosi cha kwanza baada ya Charlton mnamo 2000 kuwahi kufunga jumla ya mabao 14 kutokana na mechi nane za mfunguzi wa msimu baada ya kupandishwa daraja kushiriki kivumbi cha EPL.

Licha ya kuelekeza jumla ya makombora 25 langoni mwa Arsenal, ni manne pekee ndiyo yaliyolenga shabaha huku fataki tatu zilizofyatuliwa na Rodrigo, Bamford na Raphinha kuanzia dakika ya 79 zikigonga mwamba wa goli la wageni wao.

Bamford alishuka dimbani akijivunia kufunga mabao hadi kufikia sasa msimu huu. Mbali na Raphinha ambaye ni sogora wa kwanza raia wa Brazil baada ya Roque Junior mnamo 2003 kuwahi kupangwa katika kikosi cha kwanza cha Leeds kwenye EPL, mwanasoka mwingine aliyejituma zaidi kambini mwa Leeds ni kiungo mvamizi Stuart Dallas.

Licha ya kuanza msimu kwa matao ya juu baada ya kushinda Kombe la FA katika msimu wa 2019-20, Arsenal walioshinda mechi tatu za kwanza katika kampeni zote za msimu huu, walisalia butu dhidi ya Leeds United.

Ingawa Arteta ameimarisha safu ya ulinzi ya Arsenal, kikosi hicho kimefunga mabao tisa pekee kutokana na mechi tisa zilizopita za EPL. Hayo ndiyo magoli magoli machache zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kufunga kutokana na idadi hiyo ya mechi tangu 1986-87.

Mechi dhidi ya Arsenal ilikuwa ya tatu kwa Leeds kusajili sare tasa kati ya michuano 101 ambayo imesimamiwa na kocha Bielsa.

Tangu mkufunzi huyo apokezwe mikoba ya Leeds United mnamo 2018, kikosi hicho hakijafungwa bao katika mechi 101.

Kwa upande wao, Arsenal kwa sasa wameshindwa kufunga bao kutokana na mechi nne kati ya tano zilizopita. Waliwahi kushuhudia hali hiyo katika mechi tatu kati ya 24 za kwanza ambazo Arteta alisimamia tangu aajiriwe mnamo Disemba 2019. Kuanzia wakati huo, Arsenal wameonyeshwa kadi nyekundu mara tano, mara mbili zaidi kuliko kikosi chochote kingine kwenye EPL katika kipindi hicho cha muda.

Leeds kwa sasa wanajiandaa kuwa wageni wa Everton uwanjani Goodison Park mnamo Novemba 28 huku Arsenal wakitarajiwa kuwaendea Molde kwa minajili ya gozi la Europa League mnamo Novemba 26 kabla ya kuwaalika Wolves kwa mechi ya EPL mnamo Novemba 29, 2020.