Michezo

Arsenal warudi kwa wimbo wao wa ‘next season’ baada ya kubanduliwa UEFA

April 18th, 2024 2 min read

MANCHESTER, Uingereza

ARSENAL na Manchester City watalazimika kujaribu tena bahati yao msimu ujao kwenye kipute cha Klabu Bingwa Ulaya baada ya wote kusalimu amri katika robo-fainali Jumatano.

Miamba hao kutoka Uingereza, wangejishindia Sh1.77 bilioni kila mmoja kufika nusu-fainali.

Wanabunduki wa Arsenal waliopigwa na wenyeji wao Bayern Munich 1-0 Jumatano katika mechi ya marudiano ya robo-fainali na kuaga mashindano ya Ulaya kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mkondo wa kwanza, walitia mfukoni Sh1.5 bilioni.

Walipata kipigo cha nane mikononi pa Bayern kupitia goli la beki Joshua Kimmich katika kipindi cha pili ugani Allianz Arena.

“Tulifanya kosa moja kubwa ndani ya kisanduku na tukaadhibiwa,” akasema kocha Mikel Arteta.

Wanabunduki hao wanaoshikilia nambari mbili kwenye Ligi Kuu (EPL), walikung’utwa 2-0 na Aston Villa (nambari nne) Jumapili, watavaana na Wolves (nambari 11) kesho ugani Molineux.

Mechi zinakuja kwa fujo na nambari mbili Arsenal (alama 71) hawana nafasi ya kuramba kidonda kwani baada ya Wolves, wataalika nambari tisa Chelsea (47) ugani Emirates mnamo Aprili 23 na kufunga mwezi dhidi ya nambari tano Tottenham (60) mnamo Aprili 28.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza na viongozi City waliachilia taji la Klabu Bingwa Ulaya baada ya kupoteza dhidi ya washikilizi wa rekodi ya mataji mengi Real Madrid (14) kwa njia ya penalti 4-3 ugani Etihad, Jumatano.

Walitoka sare 3-3 ugani Santiago Bernabeu mnamo Aprili 9 na 1-1 Jumatano na kulazimu upigaji wa penalti kuamua mshindi. Luka Modric alipoteza penalti kwa upande wa Madrid nao Bernardo Silva na Mateo Kovacic wakauza upande wa City.

Madrid, ambao walibanduliwa na City katika nusu-fainali mwaka jana kwa jumla ya mabao 5-1, sasa wamefika nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya mara 33.

Naye Mwitaliano Carlo Ancelotti anayetia Madrid makali, sasa amefuzu kushiriki nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya 10, sawa na Pep Guardiola aliyeshikilia rekodi hiyo pekee yake.

City wanaongoza EPL kwa alama 73. Vijana hao wa Guardiola watavaana na Chelsea katika nusu-fainali ya Kombe la FA ugani Wembley hapo kesho. City ndio mabingwa watetezi.

Huku Arsenal na City wakigeukia EPL, Madrid sasa watalimana na Bayern nao PSG wapepetane na Dortmund katika nusu-fainali kwenye ngarambe ya Klabu Bingwa Ulaya kati ya Aprili 30 na Mei 8.