Michezo

Arsenal wasajili Thomas Partey kujaza mapengo ya Torreira na Guendouzi waliotua Atletico na Hertha Berlin mtawalia kwa mkopo

October 6th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

ARSENAL walikamilisha usajili wa kiungo matata raia wa Ghana, Thomas Partey kutoka Atletico Madrid katika siku ya mwisho ya muhula wa uhamisho wa wachezaji mnamo Oktoba 5, 2020.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 alirasimisha uhamisho wake hadi Arsenal kwa kima cha Sh6.3 bilioni. Katika kampeni za msimu uliopita, Partey aliwajibishwa na Atletico katika mechi 35 za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na akafunga mabao matatu.

Mchango wake ulisaidia Atletico ya kocha Diego Simeone kukamilisha kampeni za La Liga katika nafasi ya tatu mnamo 2019-20. Hadi alipoaagana rasmi na Atletico, Partey alikuwa amechezea kikosi hicho mara 188 tangu ajiunge nacho mnamo 2011.

Kusajiliwa kwa Partey kulifaulishwa na hatua ya kiungo raia wa Uruguay, Lucas Torreira, 24, kukamilisha uhamisho wake hadi Atletico kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Arsenal walianza kuyahemea maarifa ya Partey, ambaye amechezeshwa na Ghana mara 29, tangu mwishoni mwa kampeni za msimu wa 2019-20.

Akiwa Atletico, kiungo huyo mkabaji alisaidia waajiri wake kutia kapuni ubingwa wa Europa League mnamo 2017-18 na taji la Super Cup mnamo 2018. Mafanikio yake katika soka ya La Liga yalichochea Atletico kumpa mkataba mpya wa miaka mitano mnamo 2018 na alitarajiwa kuendelea kuhudumu ugani Wanda Metropolitano hadi Juni 2023.

“Tumekuwa tukimfuatilia Partey kwa muda mrefu. Tumefurahi sana kumsajili hatimaye na kuja kwake kutaamsha zaidi viwango vya ushindani na kuboresha safu yetu ya kati,” akasema kocha wa Arsenal, Mikel Arteta.

“Ni sogora mwenye nguvu anayeleta tajriba pevu na uzoefu mkubwa wa kucheza katika mojawapo ya klabu kubwa katika soka ya bara Ulaya,” akaongeza Arteta.

Ingawa Arsenal walikuwa wakimvizia pia kiungo Houssem Aouar, 22, kutoka Olympique Lyon, mpango wao wa kumsajili nyota huyo raia wa Ufaransa uliambulia patupu baada ya ofa yao ya pili ya Sh5.1 kukataliwa na Lyon mnamo Oktoba 5, 2020.

Torreira aliyejiunga na Arsenal kutoka Sampdoria kwa kima cha Sh3.6 bilioni mnamo Julai 2018, sasa ameyoyomea Atletico kwa mkopo baada ya kuchezea Arsenal mara 89.

Hadi walipomsajili Partey, Arsenal walikuwa wamjinasia huduma za beki mzawa wa Brazil, Gabriel Magalhaes kwa kima cha Sh3.2 bilioni kutoka Lille ya Ufaransa, Willian Borges kutoka Chelsea bila ada yoyote na Dani Ceballos kwa mkopo wa mwaka mmoja mwingine kutoka Real Madrid.

Kuja kwa Partey kulichochea Arsenal kumwachilia kiungo Matteo Guendouzi, 21, kuyoyomea Ujerumani kuvalia jezi za Hertha Berlin kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Arsenal ambao wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya Arteta, wamesajili ushindi kutokana na mechi tatu kati ya nne za mwanzo katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu. Kikosi hicho kiliambulia nafasi ya nane kwenye soka ya EPL katika msimu wa 2019-20.