Michezo

Arsenal yaadhibiwa 3-0 Luiz akila kadi nyekundu

June 18th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI David Luiz wa Arsenal alionyeshwa kadi nyekundu katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 3-0 kutoka kwa Manchester City uwanjani Etihad.

Luiz, alikuwa pia kiini cha kupatikana kwa bao la kwanza la Man-City baada ya masihara yake kumpa Raheem Sterling nafasi ya kumzidi maarifa kipa Bernd Leno.

Difenda huyo mzawa wa Brazil ambaye alitokea benchi katika kipindi cha pili kujaza nafasi ya Granit Xhaka, alifurushwa ugani mwanzoni mwa kipindi cha pili. Kuondolewa kwake kulikuwa zao la kumkabili vibaya kiungo Kevin de Bruyne aliyefunga bao la pili la Man-City kupitia penalti.

Phil Foden aliyeingia uwanjani katika dakika ya 67 alifungia Man-City bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kushirikiana vilivyo na fowadi Sergio Aguero.

Pigo zaidi kwa Man-City ni jeraha baya alilolipata beki Eric Garcia baada ya kugongana na kipa Ederson Moraes. Ilimlazimu refa kusimamisha mechi kwa kipindi kirefu kabla ya sogora huyo kuondolewa uwanjani kwa machela.

Kocha Mikel Arteta wa Arsenal alimsaza benchi fowadi Alexandre Lacazette huku akimtupa kiungo Mesut Ozil nje ya kikosi chake cha wanasoka 20.

Ushirikiano mkubwa kati ya nahodha Pierre-Emerick Aubameyang na fowadi Eddie Nketiah uliwatatiza mabeki wa Man-City katika kipindi cha kwanza kabla ya Arsenal kulemewa kabisa baada ya Luiz kuondolewa.

Kipa Leno alifanya kazi ya ziada na kupangua makombora mengi ya De Bruyne, Sterling na David Silva.

Ushindi kwa Man-City unamaanisha kwamba viongozi Liverpool wanahitaji alama sita zaidi kabla ya kutawazwa mabingwa wa EPL msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka 30.

Pablo Mari aliyekuwa akiwajibikia Arsenal kwa mara ya pili msimu huu, aliumia katika dakika ya 23. Aliondolewa uwanjani na nafasi yake kutwaliwa na Dani Ceballos anayechezea Arsenal kwa mkopo kutoka Real Madrid.