Michezo

Arsenal yaadhibu Charlton 6-0 Nketiah akifuma matatu

June 7th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

EDDIE Nketiah alipachika wavuni mabao matatu na kusaidia Arsenal kuwaponda Charlton 6-0 katika mchuano wa kirafiki uliowakutanisha mnamo Juni 7, 2020.

Kinda huyo wa akademia ambaye amejipa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta, alifunga mabao yake yote matatu katika kipindi cha pili.

Ushindi huo unatazamiwa kuwapa Arsenal hamasa zaidi kadri wanavyojiandaa kwa gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City uwajani Etihad mnamo Juni 17, 2020.

Kabla ya kushuka dimbani kupepetana na Charlton, vijana wa Arsenal walikuwa wameshiriki vipindi viwili vya mazoezi ya pamoja katika uwanja wao wa nyumbani wa Emirates bila mahudhurio ya mashabiki.

Wachezaji wengine wa Arsenal waliocheka na nyavu za Charlton ni washambuliaji matata Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette wanaotazamiwa kutua kambini mwa Real Madrid na Atletico Madrid mtawaliwa mwishoni mwa muhula huu.

Lacazette ndiye aliyewafungulia Arsenal ukurasa wa magoli kwa kuvurumisha langoni kombora kali kutoka nje ya hatua ya 18 kabla ya ushirikiano wake na Nketiah kuchangia bao la pili lililofumwa wavuni na Aubameyang kirahisi.

Nketiah alifunga bao lake la kwanza baada ya patashika kuzuka langoni pa Charlton. Goli la pili halikumwia vigumu kujaza kimiani baada ya kusalia uso kwa macho na kipa huku la tatu litokana na krosi safi aliyoandaliwa na chipukizi mwenzake, Joe Willock aliyefungia Arsenal karamu ya mabao.

Nyota wa zamani wa Arsenal, Ray Parlour amesema kwmaba mechi tisa za mwisho katika kampeni za EPL msimu huu ni muhimu sana katika kuamua jinsi Arteta akakavyopania kupanga kikosi chake kwa minajili ya mapambano ya muhula ujao hasa ikizingatiwa suitafahamu inayozingira mustakabali wa Aubameyang, Lacazette na Mesut Ozil ugani Emirates.