Michezo

Arsenal yaamini Zaha atawasaidia kukabili mahasidi ligini

May 20th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MABINGWA wa zamani wa Ligi ya Uingereza(EPL) Arsenal sasa wanasaka huduma za nyota wa Crystal Palace usiku na mchana Wilfred Zaha na hata wapo tayari kumbadilisha na wachezaji wawili pamoja kitita kikubwa cha fedha za usajili ambacho thamani yake bado haijafichuliwa.

Ripoti zinadai The Gunners wapo tayari kuipa Crystal Palace wanasoka Calum Chambers na Reiss Nelson ili kupata huduma za Zaha ambaye atakuwa tiba wa kuimarisha safu zao za kushota na kulia ambazo zimekuwa zikikosa kuhimiliwa vilivyo msimu uliokamilika wa 2018/19.

Zaha raia wa Algeria, amekuwa nyota kwenye kampeni ya msimu uliokamilika wa EPL na aliongoza Crystal Palace kuichabanga Arsenal 3-2 kwenye ya ligi iliyosakatwa ugani Emirates majuma matatu yaliyopita.

Hata hivyo, mwanadimba huyo amesema kwamba atapania kushiriki mechi za Klabu Bingwa Barani Uropa(Uefa) msimu ujao wa 2019/20.

Ili kutwaa huduma zake na kuafikia malengo yake, Arsenal italazimika kufuzu Uefa kwa kuicharaza Chelsea kwenye fainali ya Ligi ya Uropa Mei 29 baada ya kukosa kumaliza ndani ya mduara wan ne bora.

Manchester City, Liverpool na Chelsea pia wanadaiwa wanalenga kumsajili winga huyo ambaye ameibuka kipenzi cha timu kadhaa kwenye ligi mbalimbali duniani.

Zaha alisakatia Manchester United kwa muda wa miezi 18 ambapo alikuwa akilishwa benchi mara kadhaa kabla ya kutua Crystal Palace ambako ameibuka kati ya wanakabumbu mahiri.