Michezo

Arsenal yaendelea kukaa juu Europa baada ya kula sare

November 8th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

ARSENAL walilazimishiwa sare ya mabao 1-1 ugenini dhidi ya Vitoria Guimaraes SC ya Ureno baada ya Bruno Duarte kusawazisha bao la Shkodran Mustafi.

Mustafi alifunga bao lake katika dakika ya 81 kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi ya Nicolas Pepe, hatua chache kutoka langoni.

Wenyeji walisawazisha bao hilo katika muda wa majeruhi baada ya ngome ya Arsenal kushindwa kuzuia krosi kutoka upande wa kulia.

Vitoria walikaribia kupata bao la ushindi baada ya mpira kumchanganya Mustafi lakini kombora la Rochinha halikulenga wavu kwenye mechi hiyo iliyochezewa Estadio D Afonso Henriques.

“Wachezaji wangu walipigana vikali na tulikaribia kuibuka washindi. Lengo letu ni kumaliza katika nafasi ya kwanza kundi na kufikia sasa tunaendelea vyema,” alisema Emery.

“Haikuwa mechi rahisi. Tuliongoza hadi dakika ya mwisho ya mchezo lakini wakasazisha dakika za majeruhi. Tulistahili kushinda, lakini itabidi turidhike na matokeo haya ya sare,” aliongeza.

Arsenal kwa sasa inaongoza Kundi F Kwa alama 10 kutokana na mechi nne, alama nne mbele ya nambari mbili Eintratcht Frankfurt ya Ujerumani iliyozuru Standard Liege ya Ubelgiji kucheza mechi ya nne jana. Liege inashikilia nafasi ya tatu kwa alama tatu, mbili mbele ya Vitoria inayokung’uta mkia.

Mechi nyingine zote za Europa League zilichezwa Alhamisi jioni.

Mourinho

Katika habari nyingine, Arsenal imekanusha ripoti kuwa inamtaka kocha Jose Mourinho kurithi mikoba ya Unai Emery ambaye siku zkae zinahesabika kufuatia matokeo duni.

Palizuka madai kwamba Mourinho ndiye atakayekalia kiti cha Emery.

Wakati huo huo, afisa wa polisi ameshtakiwa na mauaji ya Dalian Atkinson, zamani mchezaji wa Aston Villa.

Atkinson aliyechezea Aston Villa na pia klabu ya Manchester City aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 48 mnamo 2016 baada ya kukabiliana na maaafisa wa polisi nje ya boma la babake eneo la Telford, Shropshire.

Maafisa wawili wa polisi, wanakabiliwa na mashtaka, shirika la Crown Prosecution lilisema.

Mmoja wao ameshtakiwa kwa kuua. Huenda mwenzake akashtakiwa kwa kumjeruhi marehemu, msemaji wa CPS aliongeza.

Kisa hicho kilichunguzwa baada ya maafisa hao kutoka West Maercia walilazimika kutumia chombo hatari katika juhudi zao za kumkabili Atkinson ambaye aliaga dunia mnamo Agosti 15, 2016 katika hospitali ya Princes Royal kutokana na majeraha mbali mbali mwilini.