Michezo

Arsenal yamuomba Auba kurefusha mkataba

July 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

ARSENAL wako katika hatua za mwisho za kuandaa mkataba mpya utakaorefusha zaidi kipindi cha kuhudumu kwa mshambuliaji na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang uwanjani Emirates.

Hata hivyo, italazimu Arsenal kumsadikisha nyota huyo mzawa wa Gabon kwamba wako radhi kumuunga mkono kocha Mikel Arteta kadri anavyopania kukisuka kikosi kipya kitakachorejesha hadhi ya zamani wa miamba hao wa soka ya Uingereza.

Chini ya Arteta ambaye amewataka Arsenal lolote liwezekanalo ili kumdumisha Aubameyang kambini mwao kwa kipindi kirefu zaidi, Arsenal hawawezi kabisa kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa saba-bora.

Ina maana kwamba fursa yao ya pekee ya kunogesha soka ya Europa League msimu ujao ni kuwapepeta Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Agosti 1, 2020.

Licha ya kuhusishwa pakubwa na Inter Milan, Real Madrid, Barcelona, Chelsea na Juventus, Aubameyang ameshikilia kwamba anafurahia maisha yake uwanjani Emirates na yuko tayari kushirikiana vilivyo na Arteta ili kuwafanya Arsenal kuwa wawaniaji halisi wa mataji ya haiba kubwa katika soka ya Uingereza na bara Ulaya.

Ingawa hivyo, kusalia kwa Aubameyang kunakuja na masharti ya kulipwa mshahara wa hadi Sh35 milioni kwa wiki pamoja na bonasi na marupurupu.

Kiungo Mesut Ozil ambaye anadumishwa na Arsenal kwa mshahara mkubwa zaidi uwanjani Emirates, anapokezwa mshahara wa Sh49 milioni kwa wiki.

Aubameyang ambaye anapigiwa upatu wa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa msimu wa pili mfululizo, ana mkataba na Arsenal ambao utatamatika rasmi mwishoni mwa 2020-21.

Awali, Arteta alifichua kuwa Arsenal wanasubiri kujua iwapo watafuzu kwa soka ya bara Ulaya (Europa League) muhula ujao kabla ya kutathmini uwezekano wa kutimiza baadhi ya masharti ya Aubameyang.

Mabao mawili aliyofunga dhidi ya Norwich City mnamo Julai 1, yalimweka Aubameyang katika rekodi ya kuwa mwanasoka wa kwanza kupachika wavuni mabao 50 ya EPL haraka zaidi.

Kuondoka kwake huenda kukamchochea pia mfumaji Alexandre Lacazette kuyoyomea Atletico Madrid ya Uhispania na nafasi yake kutwaliwa na mwanasoka Thomas Partey wa Atletico. Lacazette alisajiliwa na Arsenal mnamo Julai 2017 kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa, mwaka mmoja kabla ya Aubameyang kuagana rasmi na Borussia Dortmund ya Ujerumani.