Michezo

Arsenal yanyemelea Joshua Zirkzee anayesemekana kumzidi Haaland

May 4th, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

ARSENAL FC wako tayari kujitokeza kwa nguvu sokoni mara tu kipindi kirefu cha uhamisho kitafunguliwa Juni 10, 2024, kutafuta mshambulizi Mholanzi Joshua Orobosa Zirkzee anayeaminika kugharimu Sh8.6 bilioni.

Wanabunduki wa Arsenal wamehusishwa washambulizi wengi wakiwemo raia wa Nigeria Victor Osimhen (Napoli), Mwingereza Ivan Toney (Brentford) na Mswidi Alexander Isak (Newcastle).

Hata hivyo, mabingwa hao wa zamani wa Uingereza wanaaminika sasa wameamua kumakinikia mshambulizi huyo wa Bologna FC.

Kwa mujibu wa ripoti nchini Italia, Arsenal wako tayari kumwaga mabilioni hayo ya shilingi za Kenya kiasi sawa na pauni 51 milioni kusaini Zirkzee, 22, ambaye kandarasi yake ya Bologna inakatika Juni 30, 2026.

Mchezaji huyo wa zamani wa Feyenoord, Bayern Munich, Parma na Anderlecht ametoa kucha msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Italia, akidhihirisha kuwa mshambulizi aliyekamilika na huenda ndio dawa Arsenal wanatafuta kuwa katili zaidi mbele ya lango.

Hata hivyo, kuvua Zirkzee haitarajiwi kuwa rahisi kwa sababu Juventus pia wanasemekana kutafuta huduma zake wanapolenga kunyakua kocha wa Bologna, Thiago Motta. Isitoshe, Bayern pia wana kipengee cha kumnunua tena katika makubaliano walifanya walipouzia Bologna mwezi Agosti mwaka 2022.

Licha ya kuwa ameona lango mara 11 na kusuka pasi za mwisho tano zilizojazwa kimiani ligini msimu huu, Zirkzee anasemekana kuwa bora kuliko raia wa Norway, Erling Haaland anayeongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Uingereza akichezea Manchester City.

Mbali na Juve na Bayern, Arsenal pia wanaaminika kukabiliwa na ushindani mkali wa kumsaini kutoka kwa Aston Villa.