Michezo

Arsenal yanyongwa na Villa

July 22nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Mikel Arteta ameungana kuwa “msimu huu haujakuwa bora zaidi kwa kikosi chake” baada ya Arsenal kupokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Aston Villa mnamo Julai 21, 2020 uwanjani Villa Park.

Ni matokeo ambayo yanawaweka Arsenal katika ulazima wa kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu katika nafasi mbovu zaidi tangu 1995.

Chini ya Arteta, Arsenal kwa sasa hawawezi kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa saba-bora, kumaanisha kwamba hawatakuwa pia sehemu ya vikosi vitakavyoshiriki kipute cha Europa League msimu ujao iwapo watashindwa kuwaangusha Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Agosti 1 uwanjani Wembley, Uingereza.

Bao la Mahmoud Trezeguet katika dakika ya 27 liliwapa Villa alama tatu muhimu zilizowapaisha hadi nafasi ya 17 kwa alama 34 sawa na Watford ambao pia wako katika hatari ya kuteremshwa daraja kwa pamoja na Bournemouth.

Ikisalia mechi moja pekee kwa kampeni za msimu huu kutamatika rasmi, Norwich City ambao kwa sasa wanakokota nanga mkiani mwa jedwali kwa alama 21, tayari wameshushwa ngazi.

“Imelazimu kuwa chungu na vijana kuteseka kisaikolojia. Haya si matokeo mazuri kabisa kwa kikosi cha Arsenal msimu huu. Itabidi tujiimarishe na kila mmoja ajiboreshe katika kiwango cha mtu binafsi na timu,” akasema Arteta.

Chini ya kocha Arsene Wenger aliyebanduka mnamo 2017 badaa ya miaka 20 na nafasi yake kutwaliwa na Mhispania Unai Emery, Arsenal walifuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kila msimu.

Arsenal walinogesha kivumbi cha UEFA kwa mara ya mwisho mnamo 2016-17 na watajibwaga uwanjani Emirates kwa mchuano wa mwisho wa EPL msimu huu mnamo Julai 26 dhidi ya Watford wakiwa na alama tisa zaidi nje ya mduara wa nne-bora.

Mara ya mwisho kwa Arsenal kushindwa kukamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara wa sita-bora ni 1994-95 ambapo kocha mshikilizi Stewart Houston aliaminiwa kudhibiti mikoba ambayo mkufunzi George Graham alipokonywa mnamo Februari 1995. Arsenal waliambulia nafasi ya 12 mwishoni mwa msimu huo.

Kufikia sasa, Arsenal wamepoteza jumla ya mechi 10 za EPL kwa msimu wa tatu mfululizo kwa mara ya kwanza tangu wapoteze michuano saba kati ya 1981-82 na 1987-88.

Wakati wa mechi kati ya Arsenal na Villa, ndege iliyokuwa na bango lililoandikwa “Unga mkono Arteta Kroenke Nje” ilipita angani kuashiria jinsi mashabiki wanavyoshinikiza sasa umiliki wa Arsenal kubadilishwa.

Hata hivyo, Arteta alisema: “Kroenkes ambao ni wamiliki wa Arsenal, bodi ya usimamizi na mkurugenzi wa spoti wananiunga mkono kwa asilimia 100. Itawalazimu mashabiki kuniamini kwa hilo ninalolisema.”

“Tunapania kuweka mawazo pamoja na kuibuka na mpangilio utakaorejesha Arsenal wanakostahili kuwa kwenye msimamo wa jedwali. Ni kibarua kizito lakini tupo tayari kwa mtihani huo uliopo mbele yetu,” akaongeza Arteta.

Kiungo Granit Xhaka aliyeingia uwanjani katika kipindi cha pili, alilaumu wachezaji wenzake kwa mtazamo mbaya wa kuibeza Villa hata kabla ya mechi kiasi kwamba walishindwa kabisa kuelekeza kombora lolote langoni pa wenyeji wao katika kipindi cha zaidi ya dakika 90.

“Kwa maoni yangu, huwezi kuja Villa Park na kucheza namna tulivyocheza. Tungejikatia mapema tiketi ya kushiriki Europa League msimu ujao ila kwa sasa itatulazimu kushinda Kombe la FA na tutakuwa na presha kubwa dhidi ya Chelsea,” akasema Xhaka.