Michezo

Arsenal yaomba Wolves ifanye mambo dhidi ya Man City

May 4th, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

BAADA ya Arsenal kutandika Bournemouth magoli 3-0 katika uga wa Emirates Jumamosi mchana, sasa mashabiki wake wametangaza kwamba saa moja na nusu usiku watashabikia timu ya Wolves ikivaana na Manchester City.

“Tutashabikia wapinzani wa Man City kwa nguvu zetu. Atakayeumiza Man City kwa kuinyuka mechi zilizosalia tutamjengea mnara wa ushujaa nyoyoni mwetu,” akasema Seneta Maalum Karen Nyamu.

Licha ya kwamba ushindi huo wa Arsenal dhidi ya Bournemouth uliiweka juu ya jedwali kwa pointi 83 huku nayo Man City ikibakia ya pili kwa pointi 79, shangwe hazikutanda vizuri.

Shida kwa mashabiki wa Arsenal ni kwamba, wamewekwa na hali ilivyo katika ligi hiyo kuu ya Uingereza (EPL) kushabikia kwa dhati kushindwa kwa Man City zaidi ya ushindi huo dhidi ya Bournemouth.

“Hii ni kwa sababu hatuko katika hali nzuri vile. Hatuwezi tukadanganya kwamba hatuna ile tamaa ya kutawazwa mabingwa wa msimu huu. Lakini Man City haitupei nafasi ya kupumua,” amesema shabiki sugu wa Arsenal mjini Murang’a Bi Cecilia Ngugi.

Bi Ngugi alisema kwamba mabao ya Bukayo Saka katika dakika ya 45 kupitia mkwaju wa penalti na lile la Leandro Trossard kunako dakika ya 70 kabla ya Declan Rice kufanya mambo kuwa 3-0 katika dakika ya 90+7 yalikuwa matamu “lakini sio kuzidi iwapo Man City itanyukwa na Wolves”.

Hisia za Arsenal ambayo ilikuwa ikicheza ikipingwa na baadhi ya mashabiki wa Manchester United, Man City, Liverpool, Chelsea na Tottenham Hotspur ni kwamba, iwapo Man City itashinda mechi zote nne ilizobakia nazo, itatawazwa mabingwa kwa mara ya sita mfululizo.

Arsenal imebakia na mechi mbili sasa na ikizishinda zote nayo Man City ishinde zake ubingwa utaiponyoka kwa mwaka wa 21 mfululizo.

“Mungu saidia tu malaika wako mpenda Arsenal ashuke tu atusaidie kupambana na jitu hili la Man City. Mungu ukitutendea hilo tutakushukuru milele na tuwe watiifu kwa kutoa Fungu la Kumi,” akaomba mfuasi sugu wa Arsenal mjini Murang’a Askofu Yohana Gichuhi.

Man City iko na kibarua na Wolves, Fulham, Tottenham na West Ham, maombi ya Arsenal yakiwa kwamba hata ikiwezekana, ipoteze zote au itoke sare kwa zote nne.

Kwa upande wao, baadhi ya mashabiki wa Man U wamemuomba Mungu aijalie Man City ushindi ili kuepuka aibu ya kutaniwa na wenzao wa Arsenal iwapo watautwaa ubingwa.

Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro amesema kwamba “sitaki hata kufikiria Arsenal ikitwaa ubingwa huu kwa kuwa nitajihisi mgonjwa hilo likifanyika”.