Michezo

Arsenal yaongoza kwenye jedwali la EPL

June 6th, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MASHABIKI wa Arsenal kwa sasa hawashikiki baada ya timu yao kurejea juu ya jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika msimu wa 2024/25, ikiwa na pointi sufuri (0).

Kwa utani wao wa kujishasha, tayari wameanza kuposti hali ilivyo wakijigamba kwamba ‘Ndovu’ amerejea juu ya mti.

Watani wao wa jadi ambao ni Manchester United na ambao bado hawajatamatisha sherehe za Arsenal kukosa taji la EPL kwa misimu 21 mfululizo, wako katika nafasi ya 14.

Hii ni baada ya jedwali kuandaliwa lilivyo kwa kufuata mfuatano wa kialfabeti.

Baada ya kumaliza msimu wa 2023/24 katika nafasi ya pili licha ya kuwa na mwanya mzuri wa kuibuka kidedea, kwa sasa mashabiki wake ndio kusema.

“Huo ni mzaha uko nao… sitaki kujihusisha na furaha ya aina hiyo kwa kuwa kila mara msimu ukitamatika huwa tunarejea juu ya jedwali kwa lazima hadi wakati ule tutakuwa na timu EPL kwa jina Ab hadi chini ya Ar,” akasema Askofu Yohana Gichuhi wa kutoka Murang’a alipohojiwa na Taifa Spoti.

Alisema kwamba alikuwa akitarajia kwamba zile kesi za kukiuka kanuni za EPL za kudhibiti viwango vya matumizi ya pesa kwa uhamisho wa wachezaji dhidi ya klabu ya Manchester City zimeamuliwa na “ikapokonywa pointi kiasi na sisi Arsenal kutuzwa ubingwa”.

“Kumbe ni upuzi tu uko nao!” Bw Gichuhi akamwambia mwandishi huyu.

Askofu Gichuhi alisema hataki kukumbuka jinsi Man City ilivyosukuma mashabiki wa Arsenal hadi nusura wasake urogi ndio ligi iwaendee vyema.

Hata hivyo, askofu huyo alisema kwamba “hayo ni maombi mazuri na natumaini ni kwamba msimu 2024/25 tutawekwa kwa matamu ya EPL na timu hii yetu tunayoipenda kama wali kwa nyama”.

Katika jedwali hilo la kabla ya hata kipenga cha mechi ya kwanza kupulizwa, timu ya Aston Villa ambayo ndio ilisababisha Arsenal kukosa taji la 2023/24 baada ya kuitandikia kwao na pia nyumbani, iko katika nafasi ya pili.

Bournemouth na Brentford ndizo hali hii ingekuwa ya kweli wangeingia katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (Uefa) kwa kumaliza ndani ya mduara wa nne-bora.

Nazo timu za Brighton, Chelsea na Crystal Palace ndizo zingepeperusha bendera ya Europa kwa kumaliza katika eneo la saba-bora.

Timu za kuchujwa kutoka EPL kuingia Championship zingekuwa ni Tottenham Hotspur, West Ham United na Wolves.

Mabingwa wa msimu wa 2023/24 ambao ni Man City wangemaliza katika nafasi ya 13.