Michezo

Arsenal yapepeta Newcastle United na kutua mduara wa 3-bora

April 3rd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

USHINDI wa 2-0 dhidi ya Newcastle United ugani Emirates Jumatatu usiku umewawezesha Arsenal kuwapiku Tottenham Hotspur na Manchester United ambazo zilikuwa mbele yao kwa muda mrefu.

Itakumbukwa pia kwamba Arsenal haikuwahi kuwa mbele ya Tottenham tangu ligi ianze miezi minane iliyopita.

Kiungo mshambuliaji Aaron Ramsey alifunga bao la kwanza katika kipindi cha kwanza kabla ya Alexandre Lacazette kuongeza la pili, huo ukiwa ushindi wao wa 10 mfululizo uwanjani humo msimu huu.

Katika mechi zao saba zilizobakia, Arsenal itakuwa ugenini mara tano na mara mbili nyumbani, wakati huu vita vya kuwania fursa ya kumaliza miongoni mwa nne bora vikiendelea kuchacha.

Vijana hao wa kocha Unai Emery wamefikisha pointi 63, huku mashabiki wao wakiendelea kujipatia matumaini makubwa.

Licha ya kushindwa, Newcastle walicheza kwa kiwango cha juu kama kawaida yao kwenye mechi za ugenini huku wakishambulia mara kwa mara lango la Arsenal, kabla ya bao la Lacazette lililowamalizia matumaini mechi ikielekea kuisha.

Arsenal ilicheza mechi hiyo bila Laurent Koscielny na Granit Xhaka wanaouguza majeraha, pamoja na mshambuliaji matata Pierre-Emerick Aubameyang ambaye aliingia baadaye mechi ikielekea kumalizika.

Kwa hakika mpango wake wa kumuanzisha Ramsey kama nahodha ulifaulu, kabla ya nyota huyo kutolewa baada ya kuumia.

Nafasi ya staa huyo anayejiandaa kujiunga na Juventus ilichukuliwa na Aubameyang ambaye alitoa pasi iliyomwezesha Lacazette kufunga bao la pili.

Mara tu alipoingia, safu ya mbele ya kikosi chake iliimarika kiasi ya kumfanya kocha Rafael Benitez kusimama kila wakati mashambulizi yalipoanzishwa.

Ramsey afanya mashambulizi makali

Kabla ya kuona lango, Ramsey aliyeshirikiana vyema na Mesut Ozil alifanya mashambulizi makali langoni mwa Newcastle ambayo yaliwaweka mabeki wa timu hiyo katika hali ngumu daima.

Juhudi za Benitez kuwashauri mastaa wake Ayoze Perez na Miguel Almiron kutafuta bao yaliambulia patupu kutokana na ulinzi mkali wa mabeki wa wenyeji.

Emery alikuwa mwenye furaha tele akikumbuka jinsi vijana wake walichapwa na Manchester City, Chelsea katika mechi mbili za kwanza msimu huu.

“Sasa tunashikilia nafasi ya tatu. Lengo letu ni moja ingawa haitakuwa kazi rahisi. Lazima tudhihirishie kila mtu kwamba tunaweza kuendeleza ushindi wetu hadi dakika ya mwisho, ikiwa kweli tunataka kucheza mechi za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya,” alisema.