Arsenal yapoteza tumaini

Arsenal yapoteza tumaini

NA MASHIRIKA

NEWCASTLE, Uingereza

KIUNGO mahiri Granit Xhaka wa Arsenal amewashutumu wenzake wa kikosi hicho kufuatia kushindwa kwao na Newcastle United katika mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Premia (EPL) iliyochezewa St James Park, Jumatatu.

Arsenal ambao wamebakisha mechi moja waliingia uwanjani wakiwa nyuma ya Tottenham Hotspur kwa tofauti ya pointi mbili tu, huku wakifahamu vyema kwamba ushindi katika pambano hilo ungeimarisha matumaini yao ya kumaliza miongoni mwa Nne Bora na kufuzu kwa michuano ya Klabu Bingwa.

Lakini vijana hao wa kocha Mikel Arteta, walidhulumiwa, kulemewa na kushindwa kuwadhibiti na Newsatle United ambayo iliwacharaza 2-0, baada ya Ben White kufunga langoni mwake kabla ya Bruno Guimaraes kuongeza la pili.

“Najipata katika hali ngumu ya kueleza kuhusu mechi hii, tulicheza vibaya kuanzia dakika ya kwanza hadi mechi ikamalizika, na kamwe hatukustahili kuwa uwanjani,” Xhaka aliambia waandishi wa habari za michezo.

“Siwezi kueleza zaidi kuhusu mchezo wetu mbaya. Hatukucheza kulingana na mpango wa kocha, hatukufuata ushauri wa kocha na tukaamua kucheza kivyetu, na daima unapoamua kucheza kinyume na matakwa ya kocha, mambo kama haya hutokea.”

“Kilichotokea ni maangamizi. Kiwango chetu hakituruhusu kucheza katika mechi za Klabu Bingwa, na hata zile za Europa League. Ni vigumu zaidi kukubali kilichotokea, sielewi kwa nini tunapuuza ushauri wa kocha.”

“Iwapo mtu hayuko tayari kucheza, ni vyema abakie nyumbani. Mchezoni, lazima kila mtu awe tayari kucheza, licha ya umahiri wake. Unaweza kuwa na miaka 30, miaka 35, 10 au 18, kama hauko tayari, kaa kwenye benchi ama nyumbani. Usikuje hapa!

“Uwanjani, tunahitaji watu walio na ujasiri, pole kwa kutamka hayo. Lakini ni ukweli kwamba mtu anakuja uwanjani kucheza kwa kujitolea. Tumepoteza mechi iliyokuwa na umuhimu mkubwa kwetu. Lakini unapoingia uwanjani na kucheza kinyume na ushauri wa kocha, hutusaidii.

Nimesikitika zaidi kwa matokeo haya, nimeudhika sana, na kuomba msamaha kwa mashabiki waliojitokeza kutusapoti. Hatufai kwenda hivyo, naweza tu kusema poleni sana mashabiki. Sina maneno mengine ya kuongeza.”

Katika mechi ya mwisho, Arsenal watakutana na Everton ugani Emirates, lakini Tottenham watamaliza miongoni mwa Nne Bora iwapo watatoka sare na Norwich City wanaoshikilia mkia jedwalini.

Everton ya kocha Frank Lampard inakamata nafasi ya 16 kwenye jedwali na inasalia na mechi mbili pamoja na ya Arsenal ndio ikamilishe msimu huu wa ligi. Imeratibiwa kukutana na Crystal Palace kesho kabla ya kuvaana na Arsenal Jumapili.

  • Tags

You can share this post!

NJENJE: Serikali kuagiza mahindi kudhibiti bei ya unga...

Amerika kupeleka tena wanajeshi wake Somalia

T L