Michezo

Arsenal yataka Spurs ivunje Man City

May 14th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MASHABIKI wa Arsenal sasa wamenyenyekea wakitaka Tottenham Hotspur kuitwanga Manchester City Jumanne usiku katika mechi muhimu ya kuamua hatima ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Askofu Yohana Gichuhi ambaye ni shabiki wa Arsenal amesema kwamba “imani tumeweka kwamba Mungu anaweza akatekeleza mapenzi yake kwa timu hii yetu na atubariki”.

Alisema kwamba hadi sasa, Arsenal haijaonyesha dharau kwa Mungu.

“Hapa nchini Kenya, mashabiki wa Arsenal tulianza msimu huu kwa maombi tukimuomba Mungu Atujalie ushindi,” akasema Askofu Gichuhi.

Iwapo Man City itapoteza mchuano dhidi ya Spurs au watoke sare, Arsenal itakuwa na matumaini makuu ya kutwaa ubingwa.

Tofauti ya timu hizo mbili zimeachana na pointi mbili pekee ambapo Man City inapigiwa upatu mkuu wa kuibuka washindi.

Arsenal inahitaji tu Man City itoke sare au itandikwe huku nayo ikomoe Everton katika mtanange wake wa mwisho.

“Sisi tuko sasa mikononi mwa Mungu. Tutakubali matokeo. Iwapo Mungu Ameona tunafaa kutawazwa mabingwa, itakuwa hivyo. Ikiwa atatuza Man City hadhi hiyo, basi sisi tutakubali tu. Lakini katika hali zote tutaishi kuMshukuru Mungu kwa yote mema ambayo ametufanikishia katika msimu huu,” akasema askofu huyo.

Hata aliyekuwa kiungo wa Arsenal, Mjerumani Mesut Oezil, amechachisha Spurs kupitia chapisho kwa akaunti yake ya X (zamani Twitter) akiitaka kupapura Man City.