Michezo

Arsenal yatiwa adabu

September 30th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KICHAPO cha 3-1 ambacho Liverpool waliwapokeza Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Anfield mnamo Septemba 28, 2020 kilidhihirisha udhaifu mkubwa katika safu ya kati ya kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta.

Akizungumza mwishoni mwa mchuano huo, Arteta alidokeza uwezekano wa kusajiliwa kwa kiungo Thomas Partey wa Atletico Madrid au Houssem Aouar kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa ili wamsaidie Pierre-Emerick Aubameyang kubeba mzigo wa ufungaji mabao.

Nyota Aubameyang, ambaye alikuwa mwiba kwa Liverpool timu hizi zilipokutana mwishoni mwa msimu jana, alibanwa vilivyo na mabeki wa nyumbani na hakupata hata fursa ya kumbabaisha kipa Alisson Becker wa Liverpool langoni pake.

Mashabiki wa Arsenal walifurahi kuona kikosi chao kikianza vyema msimu huu mpya baada ya kushinda mechi mbili za kwanza: 3-0 dhidi ya Fulham na 2-1 dhidi ya West Ham United.

Lakini dhidi ya Liverpool, washambuliaji wa kocha Mikel Arteta walishindwa kabisa kuwika katika mechi hiyo.

Kwa mujibu wa mashabiki walioshuhudia mechi hiyo ya ugenini, itabidi Aubamayeng apewe sapoti ya kutosha kutoka kwa akina Alexandre Lacazette (aliyefunga bao la pekee la Arsenal), Willian Borges, Dani Ceballos na Nicolas Pepe.

Wanawataka wachezaji hao kuonyesha umahiri zaidi katika kumiliki mpira na pia kufunga mabao, iwapo watakuwa na matumaini yoyote ya kumaliza katika nafasi nzuri msimu huu.

Kwenye mechi hiyo Liverpool walionyesha ubabe wao walipotoka nyuma na kuandikisha ushindi huku mchezaji mpya Diogo Jota akifunga bao lake la kwanza.

Arsenal walitangulia kuona lango kupitia kwa Lacazette kutokana na makosa ya Andrew Robertson.

Hata hivyo, fowadi Sadio Mane alisawazisha dakika chache baadaye kipa Bernd Leno alipotema mkwaju wa Mohamed Salah.

Safu ya ulinzi ya Arsenal iliposinzia tena beki wa kushoto Andrew Robertson alitia kimiani bao la pili kuweka mabingwa hao watetezi kifua mbele kwenda mapumzikoni.

Liverpool walitawala mechi hiyo katika kila kiwango huku wakionyesha dalili za mapema za kuhifadhi ubingwa wao.

Licha ya kocha Jurgen Klopp kuingia uwanjani bila huduma za kiungo mgeni Thiago Alcantara na kigogo Jordan Henderson wanaouguza majeraha, hapakuwa na udhaifu wowote.

Ushindi huo uliwapaisha hadi nafasi ya pili jedwalini nyuma ya Leicester City waliowacharaza Manchester City 5-2 siku ya Jumapili.

Baada ya mechi Kloop alisifia vijana wake kwa mchezo mzuri, huku akimmiminia sifa Jota kwa mchango mkubwa licha ya kuwa mgeni kikosini.

Kwa upande wa Arsenal, mwanzo mzuri tangu wanyakue mataji mawili ya hivi punde – FA mwisho wa msimu jana na Community Shield mwanzo wa msimu huu – pamoja na ushindi dhidi ya Fulham na West Ham katika EPL kufikia Septemba 28, uliwapa mashabiki matumaini.

Lakini kikosi hicho kilidhihirisha udhaifu wake wa muda mrefu katika safu ya kiungo, ambayo ilipoteza mipira mara kwa mara na kukosa maarifa ya kusuka pasi za kupeleka timu mbele.

Ingawa hivyo, kwa mara ya kwanza katika kipindi kirefu straika Lacazette alionyesha kiwango cha juu kwa kufunga bao na kupoteza nafasi zingine mbili za wazi akiwa peke yake na kipa Allison aliyeokoa makombora yake mawili yakielekea wavuni.

Kocha Arteta alisema: “Tulicheza vizuri kwa kiwango kikubwa. Lakini ukweli ni kwamba walituzidi kimaarifa. Hilo lilionekana wazi. Kumbuka wamekuwa pamoja kwa miaka mingi, lakini nilifurahia kujitolea kwa wachezaji wangu wote uwanjani.”

Arsenal watarejea uwanjani Oktoba 1, 2020 kurudiana na Liverpool katika mechi ya Carabao Cup.

Kibarua chao ligini kitazidi kuwa kigumu watapakozuru Etihad kumenyana na Man-City, Old Trafford kuvaana na Manchester United na baadaye dhidi ya Leicester City nyumbani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO