Arsenal yatuma Kolasinac kuchezea Schalke kwa mkopo huku Arteta akilenga kutema wanasoka zaidi kambini mwa Arsenal

Arsenal yatuma Kolasinac kuchezea Schalke kwa mkopo huku Arteta akilenga kutema wanasoka zaidi kambini mwa Arsenal

Na MASHIRIKA

BEKI Sead Kolasinac wa Arsenal amejiunga na Schalke 04 ya Ujerumani kwa mkopo wa hadi mwishoni mwa msimu wa 2020-21 huku kocha Mikel Arteta akifichua kwamba kikosi hicho kinapania kupunguza idadi ya wanasoka wake muhula huu.

Kolasinac ambaye ni raia wa Bosnia-Herzegovina alianza kusakata soka ya kulipwa kambini mwa Schalke kabla ya kujiunga na Arsenal mnamo 2017.

“Hatuna uwezo wa kuwadumisha kambini baadhi ya wanasoka ambao hatuwahitaji kwa sasa katika baadhi ya idara. Wapo wanasoka ambao tutawatuma kwa mkopo kwingineko huku wengine wakiuzwa kabisa,” akasema Arteta.

“Kuondoka kwa wachezaji hao huenda kukatupa fursa ya kusajili masogora tunaolenga kuimarisha baadhi ya safu, hasa ya kati,” akaongeza mkufunzi huyo raia wa Uhispania.

Tangu atie guu uwanjani Emirates, Kolasinac amevalia jezi za Arsenal mara 113 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa Kombe la FA mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Katika kampeni za msimu huu, alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal mara moja pekee kwenye kivumbi cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) huku akiwajibishwa zaidi kwenye michuano ya Europa League na Carabao Cup.

“Kolasinac atapata nafasi ya kuchezeshwa mara kwa mara kambini mwa Schalke, hatua itakayoimarisha zaidi makali yake kabla ya kurejea ugani Emirates,” akasema mkurugenzi wa kiufundi kambini mwa Arsenal, Edu.

Mbali na Kolasinac, beki mwingine ambaye anatazamiwa kuondoka ugani Emirates ni Shkodran Mustafi ambaye ni raia wa Ujerumani. Arsenal tayari wamefichua mipango ya kuagana pia na kiungo Mesut Ozil ambaye mkataba wake unatamatika mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Nyota huyo mzawa wa Uturuki na raia wa Ujerumani aliachwa nje ya kikosi cha Arsenal kwenye kampeni za EPL na Europa League msimu huu wote.

Kati ya wachezaji ambao Arsenal tayari iliwatuma kwa mkopo kwingineko mwanzoni mwa msimu huu ni beki Konstantinos Mavropanos (Stuttgart, Ujerumani), kiungo Lucas Torreira (Atletico Madrid, Uhispania) na kiungo Matteo Guendouzi (Hertha Berlin, Ujerumani).

Chini ya Arteta, Arsenal kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 20 kutokana na mechi 16 baada ya kushinda Chelsea na Brighton mfululizo. Kikosi hicho kwa sasa kinajiandaa kuvaana na limbukeni West Bromwich Albion mnamo Januari 2, 2020.

You can share this post!

Wanaraga wa Kenya Harlequins wamdumisha Benjamin Ayimba...

Mechi za kimaeneo za kufuzu kwa fainali za Hoki ya Afrika...