Michezo

Arsenal yawafuta kazi maskauti waliochangia kusajiliwa kwa Saka, Willock na Nketiah

May 30th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ARSENAL imefuta kazi maskauti 10 waliotambua utajiri wa vipaji vya chipukizi Bukayo Saka, Ainsley Maitland-Niles na Reiss Nelson na kushawishi usimamizi kuwasajili.

Wahudumu wengine ambao Arsenal imelazimika kuwatema baada ya hazina yao ya fedha kutikiswa pakubwa na janga la corona ni vibarua ambao mikataba yao ilikuwa itamatike rasmi mwishoni mwa Juni 2020.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, wote walioathiriwa na mabadiliko hayo walifahamishwa kupitia baruapepe.

Licha ya maamuzi hayo ya ghafla, Arsenal imesisitiza kwamba itapania kuwaajiri upya wafanyakazi wake wote walioagana nao kutokana na corona baadaye mwaka huu au pindi janga hilo litakapodhibitiwa vilivyo.

Mwanzoni mwa msimu huu, Arsenal walimtimua kinara wa usajili wa chipukizi Steve Morrow katika juhudi za kusuka upya idara yao ya usimamizi.

Wengi wa makinda walioanza kuwajibishwa katika kikosi cha kwanza baada ya kuondoka kwa Morrow wamekuwa wakitamba sana ugani Emirates huku baadhi yao wakitazamiwa kuwa mhimili muhimu wa kikosi hicho katika siku za halafu.

Miongoni mwa chipukizi hao ni Nelson, Joe Willock, Eddie Nketiah na Saka ambaye kwa sasa anahemewa pakubwa na Liverpool.

Mwishoni mwa msimu jana, Arsenal walitia kapuni zaidi ya Sh7 bilioni kutokana na tukio la kuuzwa kwa makinda wao wa zamani waliopokezwa malezi ya soka katika akademia yao. Hao ni pamoja na Alex Iwobi na Krystian Bielik walioyoyomwa Everton na Derby County mtawalia.