Michezo

Arsene Wenger ajibu maswali kuhusu Arsenal, VAR, Ozil, Ronaldo na Ibrahimovic

October 20th, 2020 5 min read

Na MASHIRIKA

ARSENE Wenger ni miongoni mwa wakufunzi ambao wanakumbukwa kwa kuchangia pakubwa mabadiliko yanayoshuhudiwa kwa sasa kwenye soka ya Uingereza.

Kocha huyo alipokezwa mikoba ya Arsenal mnamo 1996 na akahudumu kambini mwao kwa miaka 22 ambapo alinyanyua mataji saba ya Kombe la FA. Pia aliongoza Arsenal kuweka historia ya kushinda taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) bila kushindwa mnamo 2003-04.

Tangu abanduke uwanjani Emirates, Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 70 alipokezwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) majukumu ya kusimamia maendeleo ya soka kimataifa.

Haya ni mahojiano ya Wenger na Shirika la Habari la BBC kuhusu mambo ya kale, ya sasa na yajayo.

Je, Arsenal ina maana gani kwako?

Nilitenga miaka 22 ya maisha yangu ili nijenge kikosi cha Arsenal. Niijenga kituo cha mazoezi na uwanja wa Emirates. Niliangusha jasho kuhakikisha kwamba fedha zilizotumiwa kujengea uga wa Emirates zinarejeshwa. Nilijitahidi kutengeneza mazingira mazuri kwa wanasoka na kuunda miundo-msingi ambayo ingetoa jukwaa zuri kwa kikosi kuwekeza ipasavyo.

Mimi ni kama mume aliyetamatisha uhusiano na mkewe kisha akanyimwa fursa ya kuonana na watoto hao anaowapenda sana.

Je, ulifanya kosa kushawishi Arsenal kuomba mkopo ili kujenga uga wa Emirates?

Nilikubali mpango huo kwa sababu nilijua ungeleta changamoto mpya. Miaka yangu 10 ya kwanza kambini mwa Arsenal ilikuwa ya kushinda mataji. Nilijua kwamba ingekuwa vigumu kushinda chochote katika miaka 10 ya baadaye kutokana na uzito wa kulipia mkopo.

Licha ya panda-shuka hizo, naamini kwamba tulicheza soka safi ya kutamanisha na kwa nyakati fulani tulikuja karibu sana kushinda mataji japo kikosi kwa ujumla kilikuwa kichanga mno.

Najivunia zaidi awamu ya pili ya ukufunzi wangu kambini mwa Arsenal kwa sababu awamu ya kwanza ilikuwa rahisi. Awamu ya pili ilikuwa ngumu na iliweka uvumilivu na kiwango cha kujitolea kwetu kwenye mizani.

Hujawahi kurejea ugani Emirates tangu upoteze kazi kambini mwa Arsenal mnamo Mei 2018…

Nimeteua kudumisha umbali kabisa. Ingawa hivyo, umbali huo ni wa kimwili tu, si wa kimawazo wala kihisia. Ni muhimu hivyo ili watu wasikuone kuwa kivuli au aliye na mpango wa kushawishi mambo fulani yafanywe kwa namna unavyofikiria na kutaka. Nilihisi kwmaba kitu bora zaidi cha kufanya ni kukatiza uhusiano huo wa karibu sana na Arsenal kwa sasa.

Mwishoni mwa kipindi chako cha ukocha Arsenal kulikuwa na maandamano ya mashabiki dhidi yako. Je, yaliathiri utendakazi wako?

Sidhani kuna uzito wowote katika kile ambacho shabiki anaweza akasema kwa wakati fulani. Shabiki husema kitu kutegemea hisia zake wakati huo. Leo hii, inaonekana kwamba ni mashabiki wachache sana ambao huamua msimamo unaochukuliwa na wengine. Mashabiki 50 pekee wakitumia mitandao ya kijamii kusema mabaya tu kuhusu mtu, upo uwezekano kwamba wanachokisema kitaathiri zaidi ya watu 60,000 uwanjani.

Hata hivyo, haimaanishi kwamba kocha lazima afanye kila kitu kinachosemwa na kila shabiki. Ukiangalia miaka mitatu ya mwisho ya ukocha wangu, Arsenal walikamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya pili, nyuma ya Leicester City. Kila kikosi kilimaliza ligi nyuma ya Leicester ambao walipoteza mechi tatu pekee. 2017 ulikuwa mwaka wa kwanza tangu 1997 kwa Arsenal kukosa kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Yalikuwa matamanio ya kila mtu kambini kuona Arsenal ikiendeleza rekodi hiyo ya kutokosa kuwa sehemu ya kampeni za UEFA. Lakini mambo hubadilika, na huenda msimu huu wa 2020-21 ukawa wao kufanya hivyo.

Uhasama ulitawala sana uhusiano wako na Sir Alex Ferguson wa Manchester United na Jose Mourinho wa Chelsea. Je, mambo bado ni hivyo? Je, nyinyi bado huwasiliana?

Ni nadra sana tuwasiliane kwa sababu mara nyingi siko nchini Uingereza. Uhasama ulikuwa mchezoni kwa sababu kanuni ya kushindana ni kwamba ni wewe dhidi ya wao. Lakini mambo huwa tofauti nje ya uwanja. Unapokutana na watu nje ya ulingo wa mchezo, uhasama hauna nafasi. Kila kocha hutesekea kikosi chake. Mara nyingine mambo huwa sawa, mara nyingine huwa magumu. Ni lazima ujitahidi utetee kazi yako licha ya panda-shuka. Kwa ujumla, sisi huheshimiana sana.

Ukiwa Arsenal, ulikata ofa mbili za ukocha kambini mwa Real Madrid, Man-United, Bayern Munich, Juventus, Paris St-Germain, timu ya taifa ya Ufaransa na Uingereza – ni ofa gani kati ya hizo ulikuwa karibu sana kuikubali?

Real Madrid kwa sababu hakuna mtu amewahi kukataa mara mbili ofa ya kuwanoa. Nilihiari kusalia Arsenal licha ya kwamba ni kikosi kilichokosa raslimali muhimu za kuniwezesha kushinda EPL au UEFA. Mapenzi ya dhati kwa Arsenal yasingeniruhusu kushawishika kubanduka.

Kuna aina tofauti za makocha. Nilikuwa mkufunzi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi kambini mwa AS Monaco na nikawa kocha aliyedhibiti mikoba ya Arsenal kwa kipindi kirefu zaidi vilevile – hiyo ni sehemu ya tabia yangu. Sipendi kuhamahama.

Ni kikosi kipi kilikuwa mshindani mgumu zaidi au ni wachezaji gani walihemesha zaidi vijana wako wa Arsenal?

Kikosi: Wimbledon nilipokuja Uingereza kwa mara ya kwanza. Wachezaji: Roy Keane na Alf-Inge Haaland – walitatiza Arsenal pakubwa kila mara tulipocheza dhidi yao.

Bila shaka una majuto ya kutowahi kusajili wanasoka wa haiba kubwa. Je, umewahi kujiuliza ingekuwaje?

Huwa najiuliza jinsi ingekuwa iwapo Cristiano Ronaldo angewahi kucheza pamoja na Thierry Henry, [Robert] Pires, [Sylvain] Wiltord and [Dennis Bergkamp] kambini mwa Arsenal. Pengine tungefunga mabao 200 kwa msimu mmoja!

Majuto ni kawaida. Mara nyingine utafikiria kwamba ni kosa lako, pengine hukuwajibika haraka iwezekanavyo, au mlikwazwa kifedha kwa wakati ufaao. Lakini hali ni hivyo kwa kila kikosi. Chelsea, Man-United, Liverpool wote watakuambia kuna wachezaji waliwahi kutamani lakini wakakosa.

Unajuta kutomsajili Zlatan Ibrahimovic baada ya kumwalika kwa majaribio?

La. Kwa sababu alikuwa na umri wa miaka 17 pekee wakati huo akichezea Malmo katika Ligi ya Daraja la Pili nchini Uswidi. Hakuna yeyote aliyekuwa akimfahamu wakati huo. Isitoshe, tuliwajaribu wanasoka wengi sana wakiwa chipukizi wa miaka 17 na ilikuwa vigumu kufanya maamuzi ya kusajili au la.

Ungependa ukumbukwe kwa lipi?

Kama mtu aliyewajibikia Arsenal kwa kujitolea sana, kwa uwazi, uadilifu na mapenzi ya dhati. Niliwapa Arsenal miaka bora zaidi ya maisha yangu.

Je, ni ukweli kwamba ratiba yako bado ni ile ile kabla ya kuacha ukocha? Je, bado unashiriki mazoezi kwa saa mbili kila siku?

Hilo ni kweli, hata wikendi. Michezo ni kama kupiga meno brashi – si kitu cha kufanywa mara moja kwa wiki. Ni kitu cha kila siku ili usalie katika ubora wako.

Unatazama mpira kwa kiasi gani sasa?

Cha pekee ambacho mimi hutazama ni kabumbu. Kila asubuhi mimi hutazama mechi za usiku uliotangulia. Hiyo ndiyo raha yangu. Unapozaliwa, msukumo wako wa kwanza duniani ni kuishi. Baada ya hapo, una jukumu la kubaini ni nini maana ya maisha. Maisha yangu ni soka.

Nilikulia katika sehemu ambapo kikosi cha soka ya mtaani kilikuwa na makao yake makuu. Nilianza kusikiliza mijadala kuhusu soka nikiwa na umri wa miaka minne au mitano. Hivyo nilikua nikijua kwamba cha muhimu zaidi maishani ni soka

Je, Arsenal wako salama mikononi mwa kocha Mikel Arteta?

Naam. Ana sifa zote za kuwa kocha bora na wa haiba kubwa. Wengi wa wachezaji niliowahi kunoa wana sifa hizo. Inabidi tuwape muda, wafanye kazi kwa namna wanavyoona kuwa bora zaidi. Arteta ni kocha mwerevu, ana mapenzi ya dhati kwa kikosi na nidhamu ya hali ya juu. Ni matumaini yangu kwamba ataendelea kuzingirwa na watu wazuri wanaomfaa.

Ulimsajili Mesut Ozil kwa rekodi ya Sh5.9 bilioni. Je, una maoni gani kuhusiana na taaluma yake kwa sasa?

Nahisi kwamba anapotezewa muda. Yuko katika miaka ambapo mchezaji mwenye kipaji kama chake anatarajiwa kuwa na ushawishi mkubwa uwanjani. Naye pia anapotezea Arsenal muda kwa sababu ana utajiri mkubwa wa talanta na ana uwezo wa kuchangia idadi kubwa ya mabao. Ni bingwa wa dunia aliyewahi kuchezea Real Madrid! Lakini soka inabadilika. Inahitaji sasa mipira mingi ya kushtukiza na pasi za harakaharaka. Kila kikosi hucheza hivyo kwa sasa na Ozil si mwanasoka wa kung’aa katika mchezo wa aina hiyo.

Umekuwa ukiunga sana teknolojia ya VAR. Mbona?

Imepunguza idadi kubwa ya maamuzi mabaya ya merafa kutoka asilimia 84 hadi 95. Ni teknolojia nzuri inayostahili kukumbatiwa na mashirikisho yote ya soka duniani.