Michezo

Arteta ala mori, United na Liverpool zikisare

April 7th, 2024 2 min read

NA JOHN ASHIHUNDU

KOCHA Mikel Arteta amesema wachezaji wake wanafanya kazi kwa bidii ya mchwa kuweka ulinzi mkali katika kila mechi, na kuwa kikosi ambacho kimefungwa magoli machache mno msimu huu wanapozidi kupaa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

“Wachezaji wanajiamini, kila mtu ako fiti kimwili na kiakili. Tuko pahali pazuri kwa sasa. Nimefurahi kweli,” alitanguliza Arteta.

“Tulikuwa wazuri sana leo. Hususan ngome yetu ya ulinzi ilikuwa thabiti,” akasema kocha huyo raia wa Uhispania.

Arteta alizungumza baada ya masogora wake kusakama wenyeji Brighton & Hove Albion 3-0, katika uwanja wa American Express (Amex) mnamo Jumamosi usiku, Aprili 6, 2024.

Ushindi ulipaisha Arsenal maarufu Gunners, hadi kileleni mwa jedwali kabla Liverpool kusakata mechi yao ya ugenini dhidi ya Manchester United uwanjani Old Trafford, Jumapili jioni, Aprili 7, 2024.

Man-United na Liverpool walitoka sare ya 2 – 2.

Arsenal sasa wamejizolea pointi 71 kutwaa uongozi wa ligi — sawa na Liverpool ila inawashinda kwa ubora wa mabao.

Mabingwa watetezi Manchester City wanafunga tatu-bora na alama 70.

Bukayo Saka alifungulia Gunners ukurasa wa mabao akitinga penalti dakika ya 33 baada ya Gabriel Jesus kuchezewa ngware katika kijisanduku cha hatari.

Juhudi za Brighton kurejea katika mechi kipindi cha pili kwa mashambulizi ziliyeyushwa na Kai Havertz alipofungia Arsenal goli la pili dakika ya 62.

Kisha Leandro Trossard akadunga msumari wa mwisho dhidi ya timu yake ya zamani kwa kutikisa nyavu bao la tatu dakika ya 86.

“Kikosi kimeimarika. Nahisi tutaendelea kupata matokeo mazuri mechi zilizobakia. Mliona jinsi walizidi kushambulia hata tukiongoza 3-0. Kila mtu anataka tushinde ligi,” akahitimisha kocha Arteta.

Katika mechi zingine Jumamosi, Luton Town ilifufuka kuandikisha ushindi wa 2-1 dhidi ya AFC Bournemouth, wakati kasi ya Aston Villa ikipunguzwa na wageni Brentford katika sare ya kusisimua ya 3-3 ugani Villa Park.

Naye Bruno Guimaraes alifungia Newcastle United bao la pekee lililotoa pumzi Fulham 1-0.Nayo matumaini ya Wolves kushinda mbele ya mashabiki wao yalizimwa na West Ham United waliowacharaza 2-1, wakati Everton ikivuna ushindi muhimu wa 1-0 dhidi ya Burnley katika mechi ambayo wageni Burnley walisalia wachezaji 10 baada ya mmoja kulishwa kadi nyekundu.