Michezo

Arteta amhimiza Pepe ajitahidi zaidi ili awe tegemeo katika kila mchuano

November 27th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta amemtaka fowadi Nicolas Pepe kuimarisha makali yake na kudhihirisha ubora wake mara kwa mara katika michuano mbalimbali.

Hii ni baada ya nyota huyo raia wa Ivory Coast kuweka kando maruerue ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchuano uliopita wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Leeds United na kusaidia Arsenal kusajili ushindi wa 3-0 dhidi ya Molde mnamo Novemba 26, 2020 nchini Norway.

Ufanisi huo wa Arsenal uliwawezesha kufuzu kwa hatua ya 32-bora ya kampeni za Europa League msimu huu.

Pepe alishutumiwa vikali na Arteta kwa kuchangia masaibu ya Arsenal walioambulia sare tasa dhidi ya Leeds United ugani Elland Road mnamo Novemba 22, 2020.

Hata hivyo, sogora huyo aliwafungulia Arsenal ukurasa wa mabao dhidi ya Molde katika dakika ya 50 kabla ya mengine kujazwa kimiani na Reiss Nelson na Folarin Balogun katika dakika za 55 na 83 mtawalia.

“Nilimsoma mapema hata kabla ya mechi. Alionyesha ishara za kutuvunia ushindi muhimu na alikuwa tayari kujitahidi kadri ya uwezo wake baada ya jaribio lake la kipindi cha kwanza kugonga mwamba,” akasema Arteta kumhusu Pepe aliyesajiliwa kwa kima cha Sh10 bilioni kutoka Lille ya Ufaransa.

Pepe amejitahidi kuridhisha kambini mwa Arsenal tangu atue rasmi uwanjani Emirates mnamo 2019. Licha ya kufunga mabao matatu kutokana na mechi nne zilizopita za Europa League, kocha Arteta amesema kwamba anahitaji mafanikio makubwa zaidi kutoka kwa sogora huyo.

“Alichangia nafasi kadhaa za wenzake kufunga mabao katika vipindi vyote viwili. Swali kubwa ni lini atafikia kiwango ambapo atakuwa sasa mchezaji wa kutegemewa zaidi, na ambaye atakuwa akisajili matokeo ya kutabirika zaidi katika takriban kila mchuano,” akasema Arteta.

Ushindi dhidi ya Molde uliendeleza rekodi nzuri ya Arsenal ambao kwa sasa wanajivunia rekodi ya kutopoteza mchuano wowote wa Europa League katika Kundi B. Mabingwa hao watetezi wa Kombe la FA wamejikatia tiketi ya hatua ya 32-bora wakisalia na mechi mbili zaidi za kutandaza kundini.

Balogun, 19, alikuwa akichezea Arsenal kwa mara ya pili katika kikosi cha kwanza na alifunga bao dhidi ya Molde baada kupata mpira kwa mara ya kwanza alipoingia ugani.

Pepe alionyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Leeds United baada ya kumpiga kwa kicha kiungo Ezgjan Alioski. Alikuwa na ulazima wa kudhihirishia wakosoajia wake vinginevyo na kunyanyua Arsenal ambao kabla ya kusajili sare dhidi ya Leeds, walikuwa wamepokeza kichapo cha 3-0 na Aston Villa ligini.

Arsenal kwa sasa wanajiandaa kuwaalika Wolves uwanjani Emirates mnamo Novemba 29 kabla ya kuwa wenyeji wa Rapid Vienna katika mchuano wao ujao wa Europa League mnamo Disemba 3, 2020.