ARTETA: Ana wiki sita tu!

ARTETA: Ana wiki sita tu!

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal yuko chini ya shinikizo baada ya wakuu wa klabu hiyo kumpa muda wa wiki sita kuandikisha matokeo mazuri la si hivyo atimuliwe.

Baada ya kupoteza mechi mbili za utangulizi ligini kwa 2-0 na 2-0 dhidi ya Brentford na Chelsea mtawaliwa, mashabiki wa klabu hiyo wameanza kumshutumu vikali Mhispania huyo kutokana na mbinu zake za ufundishaji.

Pamoja na presha hiyo ya mashabiki ambao wameanza kwenda uwanjani na mabango kusisitiza apigwe kalamu, mabosi wa klabu nao wamejitokeza na kumpa kocha huyo mechi za kujinasua kwa muda usiozidi wiki sita ili ahepe kutupiwa virago.

Mechi hizo ni pamoja na ya jana Jumatano usiku ya mchujo wa Carabao dhidi ya West Brom ambayo Arsenal ilisajili ushindi wa mabao 6-0 yakifungwa na Pierre-Emerick Aubameyang (3), Nicolas Pépé, Bukayo Saka, na Alexandre Lacazette.

Ipo imani kwamba matokeo mazuri kwenye mechi hizo yatarejesha timu hiyo katika nafasi ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Arteta alijiunga na Arsenal mnamo 2019 kuchukuwa nafasi ya Unai Emery baada ya kuwa msaidizi wa Pep Guardiola katika klabu ya Manchester City, lakini ameshindwa kuonyesha ujuzi wake pale Emirates.Licha ya kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa FA Cup mwaka uliopita, kikosi chake kimekuwa kikisuasua katika mechi nyingi, ikiwa pamoja na kushindwa kumaliza miongoni mwa tano bora.

VIRUSI VYA CORONA

Wakati huo huo, timu ya EPL zimekataa kuachilia wachezaji wajiunge na timu za mataifa yao kwa mechi za kimataifa zitakazochezwa mwezi ujao.

“Uamuzi huu umeafikiwa kutokana na hofu kwamba wataambukizwa virusi vya Covid-19,” Afisa Mkuu wa timu za EPL, Richard Master ametangaza.

You can share this post!

Equity yakana kumpa Aydin mkopo wa Sh15 bilioni

KAMAU: Masaibu ya Wakenya Arabuni yakome sasa