Michezo

Arteta ataka VAR itumiwe kuanzia hatua ya makundi ya Europa League

November 6th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta ametaka teknolojia ya VAR kutumiwa kufanya baadhi ya maamuzi muhimu katika kampeni za Europa League.

Mkufunzi huyo raia wa Uhispania alisisitiza hayo mwishoni mwa mechi ya Europa League iliyoshuhudia Arsenal wakiwatandika Molde ya Norway 4-1 kwenye Kundi B uwanjani Emirates mnamo Novemba 5, 2020.

Ushindi huo uliendeleza rekodi nzuri ya Arsenal ambao kwa sasa wanajivunia rekodi ya asilimia 100 kwenye kampeni za Europa League msimu huu baada ya kujizolea alama zote tisa kutokana na mechi tatu zilizopita.

Mabao ya Arsenal kwenye mechi hiyo yangalikuwa mengi zaidi. Refa alikataa kuhesabu goli lililopachikwa wavuni na Eddie Nketiah kwa madai kwamba alikuwa ameotea alipopokezwa krosi safi na Nicolas Pepe wakati Molde walipokuwa wakiongoza 1-0.

Tofauti na hali ilivyo kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), VAR haitumiki katika hatua ya makundi ya Europa League. Mnamo Februari 2020, vinara wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) waliidhinisha matumizi ya VAR kwenye Europa League kuanzia hatua ya mwondoano pekee (32-bora)

“Sidhani ina maana yoyote kuwa na teknolojia ambayo tumesadikisha kila mtu kuamini kuwa ni ‘msema kweli’ lakini haitumii ipasavyo katika mashindano ya viwango mbalimbali,” akasema Arteta.

“Hivyo, sielewi kabisa. Tunalalamikia refa kwa maamuzi mabaya ilhali ipo teknolojia ambayo ingerahisisha hali ya kuthibitisha tulichokuwa tukililia,” akaongeza Arteta ambaye alipokezwa mikoba ya Arsenal mnamo Disemba 2019 baada ya kutimuliwa kwa mkufunzi Unai Emery ugani Emirates.

Kwa mara ya pili katika mechi tatu za makundi, Arsenal walilazimika kutoka nyuma vilevile dhidi ya Molde baada ya miamba hao wa soka ya Norway kuwekwa uongozini na Martin Ellingsen.

Kristoffer Haugen alijifunga mwishoni wa kipindi cha kwanza kabla ya Sheriff Sinyan aliyetokea benchi katika kipindi cha pili kujifunga pia na kuwaweka Arsenal kifua mbele katika dakika ya 62. Magoli mengine ya Arsenal yalifumwa wavuni kupitia kwa Pepe na Joe Willock katika dakika za 69 na 88. Bao la Pepe lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Bukayo.

Arsenal watajikatia tiketi ya hatua ya 32-bora kwenye kampeni za Europa League muhula huu iwapo watasajili ushindi mwingine dhidi ya Molde kwenye marudiano yatakayowakutanisha nchini Norway mnamo Novemba 26, 2020. Arsenal hawakuchezesha nyota Pierre-Emerick Aubameyang, Alexandre Lacazette na Thomas Partey kwenye mechi dhidi ya Molde.

Arsenal kwa sasa wanajiandaa kuendea Aston Villa kwenye kivumbi cha EPL kitakachosakatiwa uwanjani London Stadium mnamo Novemba 8, 2020.