Michezo

Arteta atarajia makuu zaidi kutoka kwa Nicolas Pepe

November 7th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta amemtaka fowadi Nicolas Pepe kujituma zaidi, kuwazima wakosoaji wake na kuwasadikisha mashabiki kwamba alisatahili kununuliwa kwa kima cha Sh10 bilioni mnamo Agosti 2019.

Pepe aliridhisha zaidi mnamo Novemba 5, 2020 katika mechi iliyoshuhudia Arsenal wakiwapiga Molde ya Norway 4-1 katika mechi ya Europa League uwanjani Emirates.

Licha ya Arsenal kujipata chini baada ya dakika 22 pekee za mchezo, nyota huyo raia wa Ivory Coast alifunga bao na kuchangia jingine lililofumwa wavuni na Joe Willock.

Pepe kwa sasa anajivunia mabao matatu kutokana na mechi 11 zilizopita ambazo amechezea Arsenal hadi kufikia sasa msimu huu.

Kwa mujibu wa Arteta, Pepe ni miongoni mwa wachezaji wa haiba kubwa zaidi ambao Arsenal wanajivunia kwa sasa na itamlazimu nyota huyo wa zamani wa Rennes kujitahidi maradufu ili kuimarisha matokeo yake na kujiboresha katika mechi hadi nyingine.

“Anahitaji kuwa mkakavu zaidi akiwa na mpira, apige pasi za haraka na ajiamini pakubwa. Akifanya hivyo mara kwa mara kila anapokaribia kijisanduku cha wapinzani, basi atakuwa miongoni mwa wavamizi bora zaidi duniani,” akasema Arteta.

“Siri kubwa zaidi ni kwamba ashirikiane na wenzake katika safu ya mbele ili naye apokezwe mipira ya kumwezesha kufunga idadi kubwa ya mabao badala ya kujitafutia magoli,” akaongeza Arteta ambaye hadi kuajiriwa kwake na Arsenal, alikuwa kocha msaidizi wa Manchester City.

“Pepe na Willian ni wachezaji wazuri sana iwapo watashirikiana na kuoanisha mitindo yao ya kucheza. Wana kasi ya kutosha na uwezo wa kupiga chenga. Sioni sababu inayowazuia wanasoka hawa kufunga zaidi ya mabao 20 kwa pamoja katika kipindi cha msimu mmoja,” akasema Arteta.

Arsenal kwa sasa wameshinda mechi tatu zilizopita kwenye mashindano yote na wanashikilia nafasi ya kwanza kwenye kundi lao la Europa League baada ya kujizolea alama zote tisa katika raundi ya kwanza ya mechi za makundi.