Habari Mseto

Arushwa jela kwa kosa la wizi wa kimabavu

March 31st, 2024 1 min read

NA BRIAN OCHARO

MSHUKIWA mmoja ametupwa jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa kimabavu.

Bw Masha Kahindi atatumikia kifungo hicho kwa kosa alilofanya miaka miwili iliyopita katika eneo la Mkobani, Jomvu.

Hakimu Gladys Olimo alisema upande wa mashtaka ulidhibitishwa kesi dhidi ya Kahindi zaidi ya shaka.

“Mshukiwa amepatikana na hatia na atatumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani,” alisema hakimu Olimo.

Hata hivyo, mshukiwa huyo alililia mahakama imuonee huruma akisema kuwa hilo ndilo lilikuwa kosa lake la kwanza.

“Naomba mahakama hii ya ukweli na haki inionee huruma. Sijawahi kupatikana na hatia kwa kosa kama hili,” alisema Kahindi.

Hata hivyo, Hakimu Olimo alisema kosa hilo lilihitaji kifungo cha ndani ili kumrekebisha mshukiwa.

Kahindi anadaiwa kumwibia Joshua Mbula simu ya mkononi yenye thamani ya Sh1, 500 na Sh800 pesa taslimu.

Kiongozi wa Mashtaka Hilary Isiaho aliambia mahakama kuwa Kahindi alikuwa amejihami kwa panga na rungu wakati alifanya kosa hilo mnamo Oktoba 2, 2022.