Michezo

AS Roma waizima Real Madrid katika mchuano wa kirafiki

August 13th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

ROMA, ITALIA

NYOTA Gareth Bale alitokea benchi katika kipindi cha pili na kuwafungia waajiri wake Real Madrid bao katika mchuano wa kirafiki uliowashuhudia miamba hao wa soka ya Uhispania wakizidiwa nguvu na AS Roma katika mikwaju ya penalti nchini Italia.

Bale alikuwa akirejea katika kikosi cha kwanza cha Real baada ya kusalia nje kwa muda mrefu tangu uhamisho wake hadi Jiangsu Suning nchini China kugonga mwamba.

Mshindi wa mchuano huo aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti baada ya pande zote mbili kuambulia sare ya 2-2 mwishoni mwa muda wa kawaida.

Diego Perotti wa Roma na Edin Dzeko walizifuta juhudi za Marcelo na Casemiro ambao awali, walikuwa wamewaweka Real kifua mbele.

Katika penalti, Marcelo aliupoteza mkwaju wake na kuwapa Roma ushindi wa 5-4 uwanjani Olimpico.

Julai 2019 kocha Zinedine Zidane aliungama kuwa Bale alikuwa karibu sana kuagana na Real ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Celta Vigo katika mchuano wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) wikendi hii.

Bale ambaye amewahi kuwachezea Tottenham Hotspur kabla ya kurasimisha uhamisho wake hadi Uhispania kwa kima cha Sh11 bilioni mnamo 2013, angali na miaka mitatu katika mkataba wake na Real.

Matumaini ya Bale kutafuna mabilioni ya China yalizimwa na Real ambao walipania kumdumisha ugani Santiago Bernabeu.

Fowadi huyu mwenye umri wa miaka 30 alitarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Suning kwa mkataba wa miaka mitatu huku akipokezwa mshahara wa hadi kufikia kima cha Sh130 milioni kwa wiki.

Mapema Julai, Zidane aliungama kwamba Bale alikuwa pua na mdomo na kuagana na Real, na kwamba kuondoka kwake ni jambo ambalo lingeleta nafuu kubwa ugani Bernabeu.

Mambo mawili

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, maamuzi ya Real kuzuia uhamisho wa Bale katika dakika za mwisho yalichochewa na mambo mawili.

Mosi, walitaka Suning walipie ada ya kumsajili nyota huyu ambaye angali na miaka mitatu kwenye mkataba wake na Real.

Pili, ni jeraha litakalomweka nje wing’a Marco Asensio kwa kipindi kirefu katika msimu wa 2019-20.

Kukosekana kwa Asensio na Dani Ceballos aliyetua Arsenal kwa mkopo kunawaweka Real katika ulazima wa kuendelea kuyategemea maarifa ya Bale. Anajivunia kuwashindia Real mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), moja la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), moja la Copa del Rey, matatu ya Uefa Super Cup na matatu ya Kombe la Dunia.

Aliwafungia Real mabao matatu na penalti moja katika fainali nne zilizopita za UEFA na hivyo kuwanyanyulia ufalme mnamo 2014, 2016, 2017 na 2018.

Wepesi wa kupata majeraha mabaya ni jambo lililomwezesha kuwasakatia Real jumla ya mechi 79 pekee katika kipindi cha misimu minne iliyopita.

Licha ya kuzomewa mara kwa mara ugani Bernabeu, Jonathan Barnett ambaye ni wakala wa Bale alisisitiza kwamba kubwa zaidi katika matamanio ya nyota huyo lilikuwa ni kuwachezea Real hadi atakapostaafu.

Bale alikamilisha kampeni za msimu jana akisugua benchi baada ya waajiri wake kujivunia matokeo duni zaidi katika kipindi cha miaka 20.

Miamba hao wa soka ya Uhispania walipoteza mechi 12, wakajizolea alama 68 na kuambulia nafasi ya tatu huku pengo la alama 19 likitamalaki kati yao na Barcelona waliotawazwa mabingwa.

Isitoshe, Real walibanduliwa na Ajax kwenye kivumbi cha UEFA katika hatua ya 16-bora. Zidane alirejea uwanjani Bernabeu mnamo Machi na kuwa kocha wa tatu wa Real msimu jana.

Ujio wa Zidane ni jambo ambalo Barnett alikiri kwamba kuliashiria mwisho wa Bale kambini mwa kikosi hicho.