Michezo

Asante Kokoto yataja kikosi chake dhidi ya Kariobangi Sharks

December 10th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

ASANTE Kotoko Jumatatu imetaja kikosi chake cha wachezaji 18 kitakachozuru Kenya kumenyana na Kariobangi Sharks katika mechi ya raundi ya kwanza ya soka ya Afrika ya Kombe la Mashirikisho jijini Nairobi hapo Desemba 14, 2018, tovuti ya Peace FM imesema.

Mabingwa hawa mara 23 wa Ghana wanatarajiwa kufunga safari ya kuelekea Nairobi mnamo Desemba 13.

Walichabanga timu ya taifa ya Ghana ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 almaarufu Black Meteors kwa mabao 3-0 katika mechi ya kirafiki Desemba 9 ya kujiweka tayari kwa mechi ya Sharks.

Vijana wa kocha Charles Kwabla Akunnor wataalika Sharks ya kocha William Muluya uwanjani Baba Yara mjini Kumasi mnamo Desemba 22 katika mechi ya marudiano.

Kotoko ilipata tiketi ya bwerere kushiriki raundi ya kwanza baada ya Cameroon kuchelewa kuwasilisha jina la mwakilishi wake kufikia siku ya mwisho ya kufanya hivyo mnamo Oktoba 15, 2018.

Sharks ilifuzu baada ya kupepeta Arta Solar7 ya Djibouti kwa jumla ya mabao 9-1. Vijana wa Muluya walikabiliana na mabingwa mara 13 wa Kenya AFC Leopards Desemba 9 katika mechi yao ya mwisho kabla ya kukutana na Kotoko. Mechi hiyo ya Ligi Kuu ilimalizika Sharks 1 na Leopards 1 uwanjani Machakos.

KIKOSI CHA ASANTE KOTOKO:

Makipa – Felix Annan, Muntari Tagoe;

Mabeki – Amos Frimpong(captain), Augustine Sefa, Abass Mohammed, Wahab Adams, Ismali Abdul Ganiu, Agyemang Badu;

Viungo – Jordan Opoku, Umar Bashiru, Daniel Nii Adjei, Richard Senanu, Kwame Bonsu Conte;

Washambuliaji – Maxwell Baako, Sogne Yacouba, Emmanuel Gyamfi, Martin Antwi, Naby Keita.