Michezo

Asante Kotoko ya Ghana yajiandaa kulimana na Kariobangi Sharks

December 8th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara 23 wa Ghana, Asante Kotoko watajiandaa kwa mechi dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya kwa kujipima nguvu dhidi ya timu ya taifa ya soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 ya Ghana jijini Accra hapo Desemba 9, 2018.

Kotoko na Sharks zinashiriki mashindano ya daraja ya pili ya klabu za Bara Afrika almaarufu Kombe la Mashirikisho (Confederation Cup). Zitalimana nyumbani na ugenini katika raundi ya kwanza kati ya Desemba 14 na Desemba 23 mwaka huu.

Tovuti ya Ghana Soccernet imesema Alhamisi kwamba Kotoko almaarufu Porcupine Warriors, “itatumia mechi ya kirafiki dhidi ya timu hiyo ya Olimpiki ya Ghana kujipiga msasa na kurekebisha makosa kabla ya kumenyana na Sharks.”

Kotoko ilipepeta Inter Allies 3-0 uwanjani Accra Sports Stadium hapo Desemba 6 katika mchuano mwingine wa kujiandaa kukutana na mabingwa wa Kombe la SportsPesa Shield Cup na KPL Super Cup, Sharks.

Timu ya Kotoko ina uzoefu wa miaka 36 katika mashindano mbalimbali ya Bara Afrika ikiwemo kushiriki Confederation Cup mara nne baada ya kufika robo-fainali mwaka 1995, raundi ya pili mwaka 1997, finali mwaka 2004 na mechi za makundi mwaka 2008. Sharks inashiriki mashindano ya Afrika kwa mara yake ya kwanza kabisa.

Sharks inapangiwa kutumia sana mechi za Ligi Kuu kujiandaa kukutana na Kotoko. Itafungua msimu 2018-2019 dhidi ya mabingwa mara 13 wa Kenya, AFC Leopards mnamo Desemba 9. Vijana wa kocha William Muluya walipepeta Arta Solar7 ya Djibouti katika mechi ya kufuzu kushiriki raundi ya kwanza ya Kombe la Mashirikisho. Kotoko ilipata tiketi ya bwerere kusonga mbele. Haikuwa na mpinzani katika awamu hiyo baada ya Cameroon kuchelewa kutuma jina ya mwakilishi wake.

Timu ya Olimpiki ya Ghana inajiandaa kukabiliana na Togo katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika la wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 ambalo litafanyika nchini Misri mwaka 2019 na pia kutumika kuchagua timu tatu zitakazoshiriki Michezo ya Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan mwaka 2020.