Habari Mseto

Ashangaza kuiba mafuta ya kupikia na sabuni ya Sh17 milioni

March 6th, 2018 1 min read

Margaret Awino Magero akiwa kizimbani kwa wizi wa sabuni na mafuta ya kupikia yenye thamani ya Sh17 milioni. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA anayeuzia mashirika ya kimataifa bidhaa Jumatatu alishtakiwa kwa wizi wa sabuni na mafuta ya kupikia  yenye thamani ya Sh17 milioni.

Bi Margret Awino Magero alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Francis Andayi.

Awino alikanusha kupokea kwa njia ya ulaghai makatoni mia tatu ya sabuni aina ya Jamaa na mitungi 3,500 ya mafuta ya kupikia aina ya Rina kutoka kwa Bw Jeremiah Kiplangat Kendagor .

Kiongozi wa mashtaka Solomon Naulikha alisema thamani ya bidhaa hizi ilikuwa Sh14, 950,000.

Shtaka la pili lilisema alipokea lita 700 ya mafuta ya kupikia aina ya Rina yenye thamani ya Sh2,240,000 kutoka kwa Bw  Lukas  Oketch Mandagi mnano  Desemba 2016.

Alikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu.