Habari Mseto

Ashangaza kujiua baada ya kunyimwa chakula na mke

May 15th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU
 
MWANAMUME wa miaka 37 katika Kaunti ya Migori alijiua kwa kujiteketeza baada ya kuzozana na mkewe kuhusu pesa za chakula.
 
Jole Onyango kutoka kijiji cha Marindi, eneo la Suna Magharibi anasemekana kujimwagia petrol na akajichoma katika nyumba yake, kama mbinu ya kueleza pingamizi zake dhidi ya mkewe.
 
Kakake Fredrick Ouma alisema kuwa Bw Onyango alikuwa akiishi na mkewe kwa zaidi ya miaka mitano, shahidi mwingine akisema kuwa marehemu alikuwa ameuza shamba lake na kumpa mkewe pesa za kuanzisha biashara.
 
Hii ilikuwa baada ya kutengana na mkewe wa kwanza.
 
“Nilipokea simu kutoka kwa jirani yake na akaniambia kuwa kakangu alikuwa amejiua,” akasema Bw Ouma.
 
Alisema kuwa Bw Onyango walitofautiana na mkewe Jumatatu, wakati alimuitisha pesa.
 
“Mwanamke anaishi Mombasa. Wakati ndugu yangu alimuitisha pesa za kula chakula cha mchana, alimuambia atumie pesa ambazo anatumia kunywa pombe,” akasema Bw Ouma.
 
Wakati majirani walifika kujaribu kuokoa hali, moto ulikuwa tayari umesambaa, huku mlango wa chuma ukiwatatiza majirani kuuvunja ili kuingia ndani.
 
Kamanda wa polisi Migori Joseph Nthenge alisema polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho, nao mwili wa marehemu ukipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Migori Level Four.