Dondoo

Ashangaza mpenzi kuchepuka bila haya akiiga mamake

April 26th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

KAREN, NAIROBI

KIPUSA mmoja kutoka familia ya mabwanyenye mtaani hapa, alimshangaza mpenzi wake alipomfichulia kwamba alikuwa akila uroda na wanaume wengine kama afanyavyo mamake.

Mwanadada huyo alikiri kwamba amekuwa akimsaliti mpenzi wake kwa kuwalisha uroda wanaume wengine akiiga tabia ya mama yake ambaye ana mipango kadha ya kando.

Inasemekana kuwa kipusa alifichua hayo baada ya mpenzi wake kumpata akipapasana na mwanamume katika kilabu moja maarufu mtaani hapa.

Kulingana na mdokezi, mwanadada ana kazi nzuri, anaendesha magari ya kifahari na huwa ana pesa za kutosha.

“Hauwezi ukasema ni tamaa ya pesa inayomfanya kuchepuka. Pamoja na kuzaliwa katika familia ya matajiri, ana kazi ya mshahara mnono. Anamiliki biashara kadhaa na mpenzi wake pia sio mchache kwa hela,” alieleza mdokezi.

Kipusa huyo alisema hana tatizo lolote na mpenzi wake na kumsifu kama gwiji wa mapenzi na kurushana roho. Hata hivyo, alisema huwa anajipata akiiga tabia ya mama yake ambaye ana wapenzi wengi.

“Alimweleza mpenzi wake kwamba amekuwa akijaribu kuacha tabia hiyo lakini ameshindwa,” alisema mdokezi.

Mwanadada alimweleza jamaa kwamba kila wiki ni lazima awaburudishe wanaume wanne tofauti anaopatana nao kwenye vilabu.

Inasemekana kuwa jamaa alimfumania mwanadada huyo baada ya kushuku mienendo yake kwa muda.

Alipomweleza mwanadada kuwa anampatia nafasi ya kuendelea na tabia yake hadi atakaporidhika, alianza kulia akisema hawezi kuishi bila yeye.

“Alimweleza kuwa hana mpenzi mwingine na kwamba hata yeye hafurahishwi na tabia ya kushiriki ufuska,” alisema mdokezi.

Jamaa aliamua kumsaidia kupata ushauri nasaha ili aone iwapo ataweza kubadilisha tabia.

…WAZO BONZO…