Ashley Young akataa ofa ya kusalia Inter Milan na anatamani kurejea EPL kusakatia Burnley

Ashley Young akataa ofa ya kusalia Inter Milan na anatamani kurejea EPL kusakatia Burnley

Na MASHIRIKA

BURNLEY wameanzisha mazungumzo na Inter Milan kuhusu uwezekano wa kumsajili beki mzoefu raia wa Uingereza, Ashley Young.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 aliondoka Manchester United mnamo Januari 2020 na kuyoyomea Italia kuvalia jezi za Inter Milan ugani San Siro.

Alikuwa sehemu ya kikosi kilichosaidia Inter Milan kutia kapuni taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) katika msimu wa 2020-21. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza tangu 2009-10 kwa Inter Milan waliokuwa chini ya kocha Antonio Conte kutawazwa wafalme wa Serie A.

Hata hivyo, kutokana na athari za janga la corona ambalo limelamaza Inter Milan kifedha, kikosi hicho kinatazamiwa kupunguza mishahara ya wanasoka wake. Klabu hiyo tayari imetangaza ugumu wa kusajili mwanasoka yeyote wa haiba katika soko la uhamisho wa wachezaji muhula huu – jambo ambalo lilimchochea Conte kubanduka ugani San Siro mwanzoni mwa Juni 2021.

Ingawa ni matamanio ya Inter Milan kuendelea kujivunia huduma za Young, mwanasoka huyo amekataa ofa mpya ya kikosi hicho na yuko radhi kurejea Uingereza na kuingia katika sajili rasmi ya Burnley.

Mbali na Watford waliowahi kujivunia huduma zake, klabu nyingine inayowania maarifa ya Young ni Inter Miami inayoshiriki kipute cha Major League Soccer (MLS) nchini Amerika.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Serikali yasaidia wanavoliboli ya ufukweni Kenya kuwania...

Wavuvi Lamu wadai maegesho yao yamenyakuliwa