Habari Mseto

Ashtakiwa kuhamisha Sh10 milioni kilaghai kwa akaunti yake

April 2nd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA aliyepatikana na hatia ya kuiba zaidi ya Sh10 milioni kutoka kwa benki ya Commercial Bank of Africa (CBA) alitozwa faini ya Sh200,000 ama atumikie kifungo cha miezi 12 jela.

Francis Muthini Mutisya mwenye umri wa miaka 45 alihukumiwa na hakimu mkuu Francis Andayi aliyempata na hatia ya wizi wa Sh10.6 milioni kutoka kwa benki ya CBA miaka saba iliyopita.

Hakimu mkuu mahakama ya Milimani Francis Andayi alimpata na hatia, Mutisya ya kuhamisha kwa njia ya ukora kitita cha Sh10.6 milioni kutoka akaunti ya Safari Park Limited hadi kwa kampuni yake Fabs Travel Limited.

Mshtakiwa huyo alikamatwa akiendelea kutoa pesa katika tawi la benki hiyo ya CBA iliyoko Parkside Nairobi eneo la Upperhill Nairobi.

“Ijapokuwa mshtakiwa alidai hajui jinsi pesa hizo zilivyoingia katika akaunti yake, ni yeye alifanya njama za kufilisi kampuni hizo zingine,” alisema hakimu.