Habari Mseto

Ashtakiwa kujiunga na Al-Shabaab, ISIS na ISIL

June 11th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI katika mojawapo ya vyuo vya teknolojia nchini alishtakiwa Jumanne kwa kuwa mwanachama wa makundi matatu ya ugaidi.

Job Kimathi Gitonga almaarufu Khaleed almaarufu Kim aliamriwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha kupambana na ugaidi ATPU kwa muda wa siku saba kuhojiwa.

Kiongozi wa mashtaka Angela Odhiambo alimsihi hakimu mkuu Francis Andayi aamuru mshtakiwa azuiliwe hadi Juni 18 kuhojiwa na maafisa wa kupambana na ugaidi nchini.

Wakili David Ayuo anayemwakilisha mshtakiwa alipinga ombi hilo lakini mahakama ikaamuru azuiliwe kuwasaidia polisi kukamilisha uchunguzi.

Mahakama ilifahamishwa mshtakiwa alikutwa katika jengo la Norwich Union, jijini Nairobi akiwa na video, picha na taarifa za kigaidi.

Mshtakiwa alikana kuwa mwanachama wa makundi ya Al-shabaab, Islamic State of Iraq and Syria (ISIS) na Islamic State of Iraq and the Levante (ISIL) yaliyopigwa marufuku nchini.

“Utarudishwa mahakamani Juni 18 wakili wako atakapowasilisha ombi la kuachiliwa kwako kwa dhamana,” hakimu alimweleza mshtakiwa.