Habari Mseto

Ashtakiwa kumuua mpenziwe kwa kutofautiana nani alifaa kuosha vyombo

May 4th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANADADA mwenye umri wa miaka 24 ameshtakiwa kwa kumuua mpenziwe walipotofautiana kuhusu ni nani aliyefaa kuosha vyombo baada ya chakula cha jioni.

Susan Njeri Wachiuri, mahakama kuu imefahamishwa, alikosana na Kelvin Njenga Ng’ang’a usiku wa Aprili 9, 2020, katika makazi yao mtaani Tena katika Kaunti ya Nairobi.

Jaji Jessie Lessit amefahanishwa kuwa wawili hao walifarakana kabla ya mshtakiwa kujihami kwa kisu na kumshambulia Njenga.

Njenga aliaga dunia baada ya muda mchache.

Jaji Lessit amefahamishwa na viongozi wa mashtaka Winnie Moraa na Angela Fuchaka kwamba mshtakiwa hana wakili wa kumwakilisha.

“Shtaka linalokukabili adhabu yake ni kunyongwa ama kufungwa jela maisha. Unahitaji wakili wa kukutetea,” Jaji Lessit amemweleza mshtakiwa huyo.

Jaji Lessit ameamuru naibu wa msajili mahakama kuu amtafutie mshtakiwa wakili kisha akatenga kesi hiyo itajwe Alhamisi wiki hii kwa maagizo zaidi.