Habari Mseto

Ashtakiwa kunyang'anya polisi simu

September 3rd, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MVULANA aliyejifanya mwombaji alimnyang’anya simu afisa wa polisi na kutoroka.

Konstebo Stephen Kivinda aliyekuwa akiendesha gari kwenye barabara ya Tom Mboya alichomoka mbio na kumwandama Dominic Mwanzia Mwalili , mwenye umri wea miaka 16.

Cha kushangaza, Mwalili, alichomoa kisu mfukoni na kutisha kumshambulia afisa huyo wa polisi anayechunguza visa vya uhalifu jijini Nairobi (CID).

Mwalili aliyeshtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Kibera Nairobi Peter Mutua kwa wizi wa mabavu alikana alitisha kumshambulia kwa kisu Konstebo Kivinda alipomnyang’anya simu yake ya rununu iliyo na thamani ya Sh30,000.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “hata yeye aliumizwa wakati wa kisa hicho.”

Ilibidi Konstebo amchape Mwalili risasi mkononi ndipo asimshambulie kwa kisu.

Mshtakiwa alivunjwa mkono ndipo akatupa chini simu aliyokuwa anapigania kuhifadhi.

Alishtakiwa aliiba simu hiyo mnamo Agosti 22, 2020 na “ wakati wa kisa hicho akatisha alitumia nguvu kwa kumtisha na kisu mlalamishi.”

Shtaka lilisema Konstebo Kivinda alinyang’anywa simu hiyo nje ya duka la Supa la Tuskys.

Alikuwa akiendesha gari la polisi iliyowekwa nambari za usajili za uraia.

Alipopigwa risasi alianguka chini.

Kiongozi wa mashtaka hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Bw Mutua alimwachilia Mwalili kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini wa kiasi hicho.

Kesi hiyo itatajwa mnamo Septemba 15, 2020.