Ashtakiwa kutukana polisi wa kike wawili

Ashtakiwa kutukana polisi wa kike wawili

MFANYABIASHARA aliyetisha kuwapiga maafisa wawili wa polisi wanawake amekana mashtaka ya kuzua vurugu na kutumia lugha chafu kwa maafisa wa usalama.

Aliposhtakiwa mbele ya hakimu mkazi Mary Njagi, Paul Kundu alikana mashtaka dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Kundu alikabiliwa na shtaka la kuwatukana polisi kinyume cha sheria nambari 94(1).

Alishtakiwa kutenda uhalifu huo katika mtaa wa Tassia eneo la Embakasi Nairobi mnamo Novemba 30,2022.

Kundu alikabiliwa na shtaka la kuwafokea polisi hao kwa kuwaambia: “naenza wachapa na hakuna kitu ama mahali mtanipeleka, hakuna sheria mnajua…nitawafunga na niwafute kazi.”

Mshtakiwa aliwakabili Koplo Caroline Nkatha na Konstebo Caroline Sabina wa kituo cha Polisi cha Tassia.

Maafisa hao walikuwa wanashika doria walipokutana na mtoto wa Kundu mwenye umri mdogo akiendesha pikipiki.

Maafisa hao walimtuma mtoto huyo kumwita baba yake.

Baada ya Kundu kuwasili, aliwakaripia maafisa hao wa polisi kisha wakambembeleza na wakamsihi waandamane naye hadi kituo cha polisi kusuluhisha suala hilo.

Aliandikiwa makosa punde tu alipofika kituoni.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh30,000 ama alipe pesa taslimu Sh20,000.

Kesi imeorodheshwa kusikilizwa Agosti 23, 2023.

Kundu atafika kortini Januari 31, 2023 kueleza mahakama ikiwa amepewa nakala za ushahidi.

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Australia kuvaana na Argentina...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uruguay waaga mashindano licha ya...

T L