Habari Mseto

Ashtakiwa kwa kudai Matiang'i aliugua Covid-19

July 28th, 2020 2 min read

RICHARD MUNGUTI na TITUS OMINDE

MWANAMUME alifikishwa mahakamani Jumatatu kwa madai ya kuchapisha habari za kupotosha na uongo katika mitandao ya kijamii kuwa, Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi akiugua Covid-19.

Hakimu Mkuu Martha Mutuku, aliamuru kuwa mshtakiwa Isaac Kibet Yego, azuiliwe kwa siku mbili kusaidia polisi kukamilisha uchunguzi dhidi yake.

Bi Mutuku aliamuru mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) amzuilie Bw Yego kwa siku mbili badala ya 14. Viongozi wawili wa mashtaka, Jacinta Nyamosi na Irungu Gitonga waliFkuwa wameomba mshukiwa huyo azuiliwe kwa siku 14 ili uchunguzi ukamilishwe.

Ilidaiwa mshtakiwa alichapisha madai ya uongo na kupotosha katika ukurasa wake wa Facebook ujulikanao kwa jina “Daily Star.”

Mbali na mtandao huo wa Facebook, Bi Nyamosi alisema mshukiwa huyo alisambaza ujumbe huo katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

“Polisi walipomkamata mshukiwa huyu mnamo Juli 25, 2020 katika kijiji cha Ngeria karibu na mji wa Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu, walimpokonya simu zake kwa lengo la kuzichunguza zaidi katika kitengo cha uhalifu wa kimitandao,” alisema Bi Nyamosi.

Atarudishwa kortini Julai 29 kujibu mashtaka.

Kwingineko, vijana kote nchini wameonywa dhidi ya utumiaji mbaya wa mitandao ya kijamii has kwa kutumiwa vibaya na wanasiasa wenye ajenda fiche zenye ubinafsi.

Muungano wa viongozi chipukizi kutoka ukanda wa North Rift unataka vijana wanaotumiwa na wanasiasa kama hao kueneza propaganda kupitia mitandao ya kijamii kujiepusha na tabia hiyo.

Kiongozi wa muungano huo North Rift, Bw Collins Chepkalei alisema kwamba vijana wengi hawajui sheria kuhusu ujasusi na utumizi mbaya wa mtandao.

Alikuwa akiongea akiwa Eldoret mnamo Jumapili wakati wa kampeni ya uhamasishaji kwa vijana kuhusu athari za kukiuka sheria za matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

“Vijana wengi hawajui sheria juu ya utumizi mbaya wa mtandao ndio maana wanatumika kwa urahisi na wanasiasa kueneza propaganda bila kujua athari za kile wanachofanya,” akasema Bw Chepkalei.

Chepkalei pia aliwaonya wanasiasa dhidi ya kufadhili vijana kueneza kampeni za matusi na uongo mitandaoni dhidi ya wapinzani wao.

Alihimiza Tume ya Uwiano na Utengamano Nchini (NCIC) na mkurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuchukua hatua kali dhidi ya vijana kama hao pamoja na wanasiasa ambao huwadhamini.

Kiongozi huyo alisema kesi za vijana wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii zinaoongezeka katika kaunti ya Uasin Gishu ambapo siku za hivi majuzi, vijana hao wamekuwa wakilenga mbunge wa Kesses Misra Swarup na gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago.