Kimataifa

Ashtua dunia kusema aliomba mbuzi idhini kabla ya kumbaka

January 8th, 2019 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

MWANAUME aliyefumaniwa akimbaka mbuzi nchini Malawi alishangaza ulimwengu baada ya kujitetea kuwa alitangulia kwa kumwomba mnyama huyo ruhusa, kabla ya kushiriki tendo la ndoa naye.

Bw Kennedy Kambani wa miaka 21 alifumaniwa na mmiliki wa mbuzi huyo pamoja na majirani akijiburudisha kwa tendo la kitandani na mnyama huyo katika eneo la Mchinji.

Polisi walisema kuwa Bw Pemphero Mwakhulika ambaye ndiye mmiliki aliripoti kuwa kwanza alidhani kuwa Bw Kambani alitaka kumwiba mfugo wake ndipo akakimbia kutafuta msaada wa majirani, japo walipowasili walimpata akijiburudisha naye kwa mahaba.

Inspekta wa polisi Lubrino Kaitano alisema “Mmiliki alidhani Kambani alikuwa akimwiba, hivyo akajulisha watu. Wakati walipofika, walishtuka kumpata akifanya mahaba na mbuzi huyo.”

Mshukiwa alikamatwa na kufikishwa katika kituo kimoja cha polisi, ambapo alifunguliwa mashtaka ya kushiriki ngono na mnyama.

Ni katika kituo hicho ambapo anaripotiwa kudai kuwa alimwomba mbuzi idhini kabla ya ‘kulala’ naye.

Hata hivyo, bado mbuzi mwenyewe hajaripotiwa ikiwa alikuwa wa kike ama dume.

Kisa hicho kimetokea baada ya kingine cha Novemba mwaka uliopita katika taifa jirani la Zambia ambapo mwanaume mwingine kwa jina Reuben Mwamba alifungwa miaka 15 gerezani na kuhukumiwa kifungo cha kazi ngumu na mahakama moja, alipopatikana uchi wa mnyama akimbaka mbuzi mwenye mimba, katika eneo la Kasama.

Awali mwezi huo, Feselani Mcube wa miaka 33 naye alifungwa kwa kumbaka mbuzi wa jirani yake ambaye aidha alikuwa na uja uzito eneo la Winterveldt, Afrika Kusini. Jamaa huyo alipatikana na mnyama huyo katika kitanda chake.