Dondoo

Ashtuka mke kukubali ajiburudishe na kahaba

February 13th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

Kwa Muhtasari:

  • Mwanamume aligundua mkewe alikuwa akigawa asali, alipougua maradhi ya zinaa
  • Mwanamke alikiri kwamba alikuwa akirushana roho na mhudumu wa gym mara kadhaa
  • Alimwambia mumewe atafute kahaba amburudishe ili kulipiza kisasi yaishe, apate hamu ya kumshughulikia tena

BUDA wa hapa, alilazimika kutafuta ushauri nasaha baada ya mkewe kumtaka atafute huduma za kahaba kulipiza kisasi alipogundua alikuwa akirushana roho na mhudumu wa gym.

Kulingana na gazeti la The Sun, mwanamume huyo alisema aligundua mkewe alikuwa akigawa asali, alipougua maradhi ya zinaa.

“Nilipigiwa simu na daktari mke wangu alipoenda hospitali. Daktari aliniambia alikuwa na maradhi ya zinaa na kulikuwa na uwezekano alikuwa ameniambukiza,” buda huyo alisema.

 

Alishindwa kuvumilia akitomaswa

Kulingana na The Sun, mwanamke huyo alikiri kwamba alikuwa akirushana roho na mhudumu wa gym mara kadhaa. Alisema jamaa huyo alikuwa akimpapasa akimsaidia kwenye mazoezi hadi akakosa kuvumilia.

“Nilianza kumdanganya mume wangu kwamba nilikuwa na ziara za kikazi za mbali ili kuwa na wakati mzuri na jamaa huyo katika nyumba yake,” mwanadada huyo alisema. Alikiri kwamba walikuwa wakifanya mapenzi bila kinga hadi akaambukizwa maradhi ya zinaa.

“Buda alishtuka kugundua kwamba wakati mwingine, mkewe alikuwa akimwalika jamaa katika nyumba yao akiwa kazini,” lilisema The Sun.

 

‘Tafuta kahaba akuburidishe’

Alisema walipatiwa dawa na mkewe akaomba msamaha. “Nilikuwa nampenda mke wangu lakini hamu ya kufanya mapenzi naye ilipungua. Aligundua hayo na kuniambia nitafute kahaba aniburudishe ili kulipiza kisasi yaishe nipate hamu ya kumshughulikia tena,” buda alisema.

Alisema pendekezo la mkewe lilimshtua sana kwa sababu maishani mwake hakuwa amefanya mapenzi na mwanamke mwingine na ikabidi atafute ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu ambao walimwambia asikubali wito wa mkewe.