Michezo

ASHUKA BEI SH4B: Coronavirus yashusha bei ya Pogba kwa Sh4 bilioni

April 25th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER United imetangaza kukata bei ya Paul Pogba kuwa Sh9.2 bilioni kabla ya kipindi kijacho cha uhamisho, tetesi zinadai.

Katika msimu wote wa 2019-2020, Pogba amekuwa akihusishwa na Real Madrid (Uhispania) ama Juventus (Italia) kwa ada ya Sh13.2 bilioni.

Hata hivyo, kutokana na athari za janga la virusi vya corona kwa uchumi katika sekta nyingi, klabu nyingi zinatarajiwa kubadilisha misimamo yao kuhusu ada ya wachezaji kulingana na hali ilivyo sokoni.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Star, hali hii imesukuma United kujiandaa kutafuta mapato kwa kuuza mshindi huyo wa Kombe la Dunia, ambaye Inter Milan inaaminika iko tayari kutoa Sh9.2 bilioni kupata huduma zake.

Mfaransa huyo amekuwa mkekani kwa kipindi kirefu msimu huu akiuguza jeraha la kifundo. Ameshiriki mechi nane pekee katika mashindano yote msimu huu.

Ingawa United inaruhusiwa kuongeza kandarasi ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 kwa miezi 12, haijaonyesha dalili iko tayari kutumia kikamilifu kipengee hicho kilicho katika kandarasi yake.

Aidha, licha ya kuwa nje kwa kipindi kirefu msimu huu, Pogba bado anasalia maarufu kwa wachezaji wenza. Anapokuwa sawa, Pogba ni mmoja wa wachezaji waliojaliwa na talanta ya hali ya juu kwenye kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Hata hivyo, majeraha yamefanya atumiwe kwa uchache na miamba hao msimu huu. Kukosekana kwa Mfaransa huyo kumeshuhudia safu ya kati ya United ikikosa ubunifu. Hali hiyo iliimarika kidogo pale United ilinunua Bruno Fernandes kutoka Sporting Lisbon mwezi Januari.

Fernandes alionyesha weledi wake kwenye Ligi Kuu kabla ya mashindano kusimamishwa mwezi uliopita kwa muda usiojulikana kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Mashabiki wengi wa United wanatamani sana kuona matunda yatakayoletwa kwa kuchezesha Fernandes na Pogba pamoja katika safu ya kati.