Makala

'Asilimia kubwa ya mishahara ya wafanyakazi mijini huishia kwa mahitaji ya kimsingi'

January 24th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

SERIKALI itahitajika kubuni sera mwafaka ili kuwezesha viwango vinavyofaa vya mishahara ya wafanyakazi wanaoishi mijini na katika sekta ya umma huku Kenya ikiorodheshwa miongoni mwa mataifa yenye viwango vya juu zaidi vya mishahara barani Afrika.

Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia, wafanyakazi nchini Kenya hulipwa mara mbili zaidi ya jumla ya uzalishaji (GDP) nchini, huku karibu asilimia 50 ikiishia katika kugharimia chakula, makao, na usafiri hasa kwa wanaoishi mijini.

Ripoti hiyo ambayo imejiri huku Wakenya wakisakamwa na ukosefu wa ajira na mishahara duni ilionyesha vilevile kwamba, katika kiwango chochote cha Jumla ya Uzalishaji Nchini (GDP), gharama ya mishahara ni ghali zaidi kwa viwanda vya uzalishaji barani Afrika.

Kutokana na hali hiyo, Kenya inakabiliwa na tishio la kukosa soko kimataifa katika sekta ya uzalishaji kutokana na viwango visivyofaa vya mishahara ya wafanyakazi nchini vinavyolemaza ushindani wa taifa hili katika soko la kimataifa.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa kwa mara ya kwanza kuhusu Biashara kwa Maendeleo katika kizazi cha Misururu ya Thamani Ulimwenguni (GVC), ilitaja viwango vya juu kupindukia vya ubadilishanaji wa hela kama kiini mojawapo cha mishahara hiyo ghali.

Katika kukabiliana na tatizo hilo, Benki ya Dunia inapendekeza kurekebisha sera kali za kudhibiti leba pamoja na kuhakikisha ulinzi wa wafanyakazi.

“Ili kupata kiwango kinachofaa cha mishahara panahitajika sera zinazopita kiwango cha leba ili kuimarisha huduma za mijini na umma. Serikali pia ni sharti ziangazie vikwazo vingine vinavyolemaza mazingira ya uwekezaji kama vile miundomsingi duni na ujuzi, vinavyoongeza gharama ya mishahara kwa kulemaza ukuaji wa uzalishaji. Huku mataifa yakilenga kujiboresha katika GVC, vigezo vya sera vinavyopatiwa kipaumbele vinaegemea ubora badala ya wingi wa wafanyakazi. Uzalishaji bora unahitaji ujuzi wa hali ya juu na uzoefu,” alisema Rais wa Benki ya Dunia David R. Malpass, kupitia ripoti hiyo.

Utafiti huo uliohusisha kampuni 5,500 kutoka mataifa 29 ulidhihirisha kwamba katika viwango vyovyote vya GDP, gharama ya leba ni ghali zaidi kwa viwanda vya uzalishaji barani Afrika isipokuwa tu Uhabeshi iliyo na viwango vinavyofaa vya mishahara.

Aidha, ripoti hiyo ilisema kuwa, kutokana na gharama ya juu ya leba, mataifa barani Afrika huongeza bei ya rasilimali zake ili ziambatane na bei ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Hatua hii huwa kikwazo kwa wawekezaji wa kimataifa wanaomiliki viwanda vinavyohitaji wafanyakazi wengi huku wawekezaji kutoka Kenya wakilazimika kuagizia bidhaa kutoka nje ili kufidia bei ghali ya mishahara katika mataifa yao.

Maadamu wawekezaji wa kimataifa hupendelea mataifa yenye usawa kati ya mishahara na kazi inayofanywa, Kenya huenda ikajipata mashakani katika kuvutia bidhaa kwenye soko la kimataifa endapo suala la viwango vya mishahara halitaangaziwa.

Kulingana na Benki ya Dunia, tatizo hili la viwango vya mishahara huathiri zaidi mataifa yanayoegemea rasilimali asilia na kugeuka tishio baada ya mataifa haya kuhamia katika misururu ya kimsingi ya thamani ya uzalishaji.

“Ni muhimu kuwa na usawazishaji. Tofauti hiyo haipo tu katika viwango vya mishahara bali pia malipo kuhusiana na GDP. Ni muhimu kuiga mataifa mengine katika viwango sawa vya maendeleo kama vile Uhabeshi na Bangladesh,” alisema Mtaalam Mkuu wa Masuala ya Kiuchumi katika Benki ya Dunia Pinelopi Goldberg.