Makala

Asimulia jinsi nusra ‘avunwe’ figo Saudia

Na OSCAR KAKAI June 25th, 2024 2 min read

EMILY Cherop Kaptui, Mkenya aliyekuwa amekwama Saudi Arabia amerejea nchini na kusimulia yaliyojiri.

Emily amekuwa akifanya kazi ya uyaya Saudia kuanzia 2021.

Mwaka huu, 2024, aliugua na kusalia kufungiwa kwa muda wa wiki moja kwenye nyumba kufuatia mahangaiko aliyopitishwa.

Mama huyu wa watoto watatu, alipata fursa ya kurejea nchini baada ya Taifa Dijitali kuangazia masaibu yake kutokana na video iliyofichuka, ikasambaa mitandaoni ikionyesha madhila aliyopitia.

Kwenye mahojiano ya kipekee nyumbani kwake kijiji cha Ekegoro, Kaunti ya Trans-Nzoia, ambako ameoleka, Emily alisimulia kwamba watoto wa mwajiri wake walitaka ‘kumvuna’ figo.

“Ninashukuru Mungu nimerejea nyumbani nikiwa hai.  Nilikuwa nikimuomba usiku na mchana aniokoe,” Emily alielezea.

Masaibu yalikuwa kibao, kiasi cha kupigana vita vikali na makundi ya watu waliotaka kumuangamiza.

Emily, 27, ambaye alikuwa akifanya kazi ya boma – uyaya katika taifa hilo la Uarabuni, anasema alifungiwa ndani ya nyumba kwa muda wa wiki moja, simu yake na stakabadhi muhimu za usafiri zikatwaliwa na mawimbi ya mawasiliano yakakatizwa.

Mahangaiko aliyopitishwa anasema yalichochewa na maamuzi yake ya kutaka kurejea nchini, hatua iliyomkera mwajiri wake.

Emily aliondoka nchini Novemba 8, 2021 kwa minajili ya kusaka ajira kukithi familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

“Wakenya na wahisani wema, likiwemo shirika la Habari la Nation Media, ninawaenzi na kuwashukuru sana kwa kuniokoa,” anasema.

Ubalozi wa Kenya Saudia ulichukulia suala lake kwa uzito na kuhakikisha amerejea nchini, baada ya kuangaziwa.

Kandarasi yake ilitamatika Novemba 2023, na kwa sababu ya bidii za mama huyu aliombwa kuiongezea.

Muda wa pasipoti yake kuwa Saudia pia ulikuwa umetamatika.

“Nilizungumza na mume wangu na akaniruhusu kuendelea kuhudumu, kwa sababu nilihitaji karo ya watoto wetu na kumaliza kujenga. Aliitikia ombi langu,” anafafanua.

Mambo yalibadilika mwajiri alipogeuka kuwa binti ya mwenye boma, ambapo Januari 2024 walihamia mji tofauti na aliotangulia kufanya kazi.

Njia za mawasiliano, Emily anaambia Taifa Dijitali kwamba zilikatizwa kabisa.

“Isitoshe, chakula nilikuwa nikipata mara moja kwa siku,” anakumbuka.

Kulingana na Mkenya huyu ambaye kwa sasa ana kila sababu ya kutabasamu, alipougua mwajiri wake mpya alikuwa anakataa ameze dawa.

Anasema shabaha ilikuwa kumuangamiza na kuvuna figo yake.

Ni katika jaribio la kutaka kutekeleza uhaini Emily anasema alipambana nao ‘kiuanaume’, akaishia kujipata hospitalini akiwa hana mbele wala nyuma.

“Ilibainika baadaye walikuwa wamebadilisha uraia wangu, na kuwa mfanyakazi aliyetoka Afrika Kusini,” anadokeza.

Katika mapambano yote Emily anasema alipopata nafasi ya kuwa na simu alikuwa akirekodi na ithibati alizokusanya ndizo zilimsaidia kurejea nchini.

Huku akiridhia kurejea Kenya, taifa analosifia kusheheni amani licha ya siasa kupamba moto na gharama ya maisha kuendelea kupanda, anasaka kazi ili kujiendeleza kimaisha.
[email protected]