Habari Mseto

Asimulia mahakama daktari alivyobeba moyo na figo ya maiti

June 26th, 2019 2 min read

Na CHARLES WANYORO

DAKTARI Jumatano alieleza mahakama ya Meru jinsi aliyekuwa mpasuaji mkuu wa maiti, Dkt Moses Njue alivyochukua moyo na figo za mfu bila idhini ya familia ya marehemu.

Dkt Scholastica Kimani, ambaye ni mpasuaji maiti katika Hospitali ya Meru Level Five, alimwambia Hakimu Mkuu Mkazi, Bw Evans Mbicha jinsi Dkt Njue alifunganya sehemu hizo za mwili wa marehemu Benedict Karau kisha akaenda nazo.

Dkt Kimani alikuwa anawakilisha serikali katika upasuaji wa mwili wa Mzee Karau, naye Dkt Njue alikuwa ameajiriwa na Bi Martha Gakou, ambaye ni mjane wa tatu wa marehemu.

Alisema Dkt Njue, ambaye aliandamana na wanafunzi kadhaa kutoka taasisi ya Kings College, waliandikisha chanzo cha kifo kuwa ni mshtuko wa moyo uliosababishwa na mgando wa damu kwenye mshipa, na kusisitiza kwenda na moyo huo ili kufanya uchunguzi zaidi wa kuthibitisha kiini hasa cha kifo.

Dkt Kimani alisema alianza kushikwa na wasiwasi kwa sababu Dkt Njue alichukua sehemu hizo za mwili bila idhini ya familia ya marehemu.

Aliongeza kuwa ingawa Mzee Karau alikuwa na majeraha kichwani yaliyoonekana wazi, hilo halikuchukuliwa kama uwezekano wa kusababisha kifo chake.

Kabla kesi ianze kusikilizwa jana, Bi Gakou alikuwa ameomba kesi iahirishwe ili wakili wake awepo.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulifanikiwa kupinga ombi hilo na kusema mashahidi saba walikuwa tayari wametoa ushahidi wao ilhali wakati huo wote hakuonyesha nia ya kutaka kushiriki kwenye kikao hicho cha uchunguzi.

Wakili wa serikali, Bw Anthony Musyoka pia alisema mahakama ilikuwa haijatoa uamuzi wake kuhusu kama kuna yeyote anayefaa kushtakiwa kuhusiana na kifo cha Mzee Karau.

Dkt Kimani alisema walituma chembe za mwili wa marehemu kwa mwanakemia wa serikali kwani ilishukiwa kulikuwa na uwezekano kifo kilisababishwa na sumu.

Dkt Njue alishtakiwa kwa madai ya kuiba sehemu hizo za mwili na kuvuruga ushahidi. Familia ya marehemu inadai hatua hiyo ilinuiwa kuficha ukweli kuhusu kiini halisi cha kifo Bw Karau.