Michezo

Asiya atashiriki Olimpiki Tokyo michezo ikiendelea

March 24th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

ASIYA Mohammad Sururu aligura kufundisha shuleni na kujitosa katika michezo mwaka 2015.

Sasa, mchezaji huyo yuko katika orodha ya Wakenya 87 waliofuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki 2020 mjini Tokyo, Japan.

Asiya anashiriki michezo ya walemavu ya tenisi, badminton na upigaji wa makasia.

Ufanisi wake wa hivi punde ni wa kushiriki Olimpiki ya walemavu.

Aliupata Oktoba 2019 alipojikatia tiketi ya kuelekea nchini Japan kwa kushinda mashindano ya kufuzu ya Bara Afrika yaliyofanyika nchini Tunisia.

Wakati huo, Asiya alikuwa mwenye furaha tele kupata ufanisi huo.

Hata hivyo, ndoto yake ya kushiriki michezo hiyo ya kifahari kwa mara ya kwanza kabisa imo hatarini kutokana na virusi vya corona, ambavyo vinakosesha dunia nzima usingizi.

“Virusi vya corona vimeumiza sana wanamichezo. Wengi wetu tulikuwa tumezamia mazoezi na kuwa fiti kimwili. Pia, wengi tu walikuwa wanashiriki mashindano. Hata wanariadha wetu kama Eliud Kipchoge walikuwa tayari kuelekea bara Ulaya kushindana,” anaeleza.

Akaongeza, “Hata hivyo, mambo yaligeuka mara moja, na kwa ghafla, hatuwezi kufanya mazoezi wala kushindana kwa sababu ya virusi vya corona. Athari ya kuacha kufanya mazoezi kwa ghafla ni kuwa mtu anaingiwa na uchovu sana.”

Siku moja tu kabla ya Machi 13 wakati serikali ilithibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya corona humu nchini, Asiya alikuwa anajiandaa kuelekea nchini Ureno kwa mazoezi. Fursa hiyo sasa haipo.

“Ilikuwa fursa yangu ya pekee kujiandaa kwa michezo ya Tokyo kwa sababu hatukuwa tumeanza matayarisho yoyote nchini Kenya.”

Anasema ratiba ya maandalizi hayo, ambayo yangefanyika mjini Aves, ilikuwa ya miezi mitatu.

Asiya hawezi kusafiri nchini Ureno kwa sababu kama tu Kenya, mataifa mengi yameweka vikwazo vya usafiri yakihofia kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, ambao umeua watu 14, 700 na kuathiri watu 340, 000 moja kwa moja.

Jumapili, visa vya corona viliongezeka nchini Kenya kutoka saba hadi 15, huku hali ya 300 ikifuatiliwa kwa karibu.

Hali hii, ambayo imeshuhudia shughuli nyingi zikisimama ikiwemo michezo, inamaanisha kuwa Asiya hawezi hata kufanya mazoezi. Siku yoyote ya kawaida, Asiya, ambaye atasherehekea kufikisha umri wa miaka 28 Aprili 25, 2020, angekuwa katika kidimbwi cha Tudor mjini Mombasa akifanya mazoezi yake.

Asiya alisoma katika Shule ya Msingi ya Port Reitz mjini Mombasa na Shule ya Upili ya Joyton mjini Thika kabla ya kusomea ualimu katika Chuo cha Walimu cha Shanzu.

“Nilifundisha katika akademia ya Shappa mwaka 2013 na 2014, lakini niliacha kwa sababu nilipenda michezo zaidi kuliko ualimu,” anasema, ingawa sasa huenda akasubiri kwa muda mrefu kutimiza ndoto ya kushiriki Olimpiki.