Habari za Kitaifa

Askari rungu 20,000 hatarini kupoteza ajira, vyama vyao vyalia

February 8th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

VYAMA viwili vya walinzi nchini, vimeonya kuwa walinzi 20,000 wako kwenye hatari ya kupoteza ajira zao, baada ya serikali kufutulia mbali leseni za kampuni tisa za kutoa huduma za ulinzi nchini.

Mnamo Jumatano, Chama cha Kitaalamu na Usalama Kenya (PSSA) na Mungano wa Sekta ya Ulinzi (PSIA), vilisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa bila taratibu zifaazo kuzingatiwa.

Vyama vilisema kuwa mnamo Februari 5, Mamlaka ya Kudhibiti Usalama wa Kibinafsi (PSRA), ilichukua hatua hiyo bila kutoa onyo au sababu zozote halisi.

Vilisema kuwa kampuni zilizoathiriwa zilikuwa zimezingatia masharti yote yaliyowekwa, jambo lililozowezesha kupewa leseni ya kuhudumu ya miaka mitano.

Vilisema kwamba kati ya kampuni tisa zilizoathiriwa, mbili zilikuwa zikingoja leseni zake kutoka.

Tangazo la kufutiliwa mbali kwa leseni hizo lilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa PSRA, Bw Fazul Mahamed.

Hatua hiyo inajiri wakati kampuni za ulinzi zimekuwa zikilalamikia agizo la PSRA kwamba zinafaa kumlipa kila mlinzi mshahara wa Sh30,000 kila mwezi, japo agizo hilo likafutiliwa mbali baadaye na Waziri wa Leba, Bi Florence Bore.

Kampuni zilipinga vikali agizo hilo, zikisema kuwa matumizi yake kwa kila mlinzi yangeongezeka hadi Sh45,000 kwa mlinzi wa mchana na Sh55,000 kwa mlinzi wa usiku.

Zilisema hazingeweza kumudu gharama hizo

“Ikiwa agizo hilo litatekelezwa, basi kuna hatari walinzi kati ya 500,000 na 700,000 wakapoteza ajira zao,” vikaeleza.

Vilionya kuwa huenda hilo likachangia ongezeko la uhalifu na wizi kutokana na upungufu wa walinzi.

Vilieleza kushangazwa kwake na ufutiliaji mbali wa leseni hizo, vikisema  “unazilenga kampuni tu zenye walinzi wengi”. Pia, vilisema kuwa serikali imekuwa ikiwalenga viongozi wanaopinga baadhi ya maagizo yake.

“Licha ya hayo tumeanzisha juhudi za kufanya mazungumzo na serikali ili kusuluhisha  mzozo huo,” vikaeleza.